Na Lydia Lugakila, Bukoba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji aliyetambulika kwa jina la Paschal Kaigwa Mariseli (21) mzaliwa wa Kijiji cha Katerero, Kata ya Kishogo, Wilaya ya Bukoba aliyekuwa akiishi na Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing Kata Rwamishenye Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Kijana huyo amekuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi Mkoani Kagera kwa kushirikiana na Wananchi ambao wamekuwa wakimsaka Kijana huyo kila chocho baada ya kutekeleza mauaji ya Bi Khadija Ismail (29) ambaye alikuwa ni Mke wa Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing Kata Rwamishenye mnamo Februari 13, 2023 majira ya saa 12 na nusu jioni kwa kumpiga na ubao kisha Kumbaka na kutokomea kusiko julikana.
Akiongea na Waandishi wa Habari leo Februari 21, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera ACP William Mwampagale amesema mtuhumiwa huyo kwa kipindi alichotoweka alikwenda kujficha vichakani na ndipo Februari 19, 2023 majira ya saa 10 jioni aliamua kutoka mafichoni baada ya kuhisi njaa kali.
Kamanda amesema baada ya kuhisi hali hiyo aliamua kwenda kutafuta msaada wa chakula nyumbani kwa Shangazi yake katika mtaa wa Kashai Manispaa ya Bukoba na baadae kukutana na watoto wa Shangazi yake ndipo Majirani wakamtambua na kisha kupiga Kelele na na kufanikiwa kumkamata.
Aidha Kamanda Mwampagale amewashukuru Wananchi wote Mkoani humo kuendelea kutoa ushirikiano Katika kuwafichua wahalifu.
Hata hivyo ametoa onyo kwa wote wanaojihusisha na vitendo mbali mbali vya uhalifu ikiwemo mauaji, ubakaji na ukatili kuacha mara moja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇