LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 20, 2023

MVUA YA MAWE YAHARIBU EKARI 15 ZA TUMBAKU SIKONGE


Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian aliyeambatana na Viongozi mbalimbali akiangalia baadhi ya mashamba ya tumbaku ya wakulima wa chama cha msingi Ngulu, katika kijiji cha Kipanga, Kata ya Chabutwa wilayani Sikonge yaliyoharibiwa na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha juzi wilayani humo. Picha na Allan Kitwe

Na Allan Kitwe, Sikonge 

MVUA kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha juzi Wilayani Sikonge Mkoani Tabora imeacha simanzi kubwa kwa wakulima wa tumbaku katika kijiji cha Kipanga, kata ya Chabutwa baada ya kuharibu zaidi ya ekari 15. 

Wakielezea tukio hilo kwa masikitiko makubwa mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian baadhi ya wakulima ambao mashamba yao yameharibiwa vibaya na mvua hiyo walieleza kuwa wamepata hasara kubwa. 

Mshara Kitoli, mkulima mkazi wa kijiji hicho alisema alikuwa amelima ekari 7 za zao hilo na alitarajia kuvuna zaidi ya kilo 500 lakini mvua hiyo imemharibia mipango yake baada ya ekari 4 kuharibiwa vibaya. Mhanga mwingine Samson Brighton, mkulima mkazi wa kijiji hicho alisema kati ya ekari 5 alizolima msimu huu ekari 4.5 zimeharibiwa vibaya na majani yote ya mmea huo yametobolewa na kuangushwa chini. Alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa wana majonzi makubwa, kwa kuwa walitarajia kupata kilo nyingi msimu huu kutokana na maandalizi mazuri ya mashamba yao, kulima kwa wakati na kupata mvua za kutosha, lakini sasa furaha yao imegeuka kuwa huzuni. 

Mwenyekiti wa Chama Msingi Ngulu (Ngulu Amcos) kilichoko katika kijiji hicho Gile Cheja, alisema mvua hizo zimeathiri AMCOS hiyo kwa kiasi kikubwa sana kwani walilima jumla ya ekari 75 za zao hilo lakini ekari 15 zimeharibiwa vibaya. ‘Tumepata hasara kubwa kwa uharibifu huu, sijui itakuwaje, tunaomba serikali iangalie namna ya kutusaidia, tuna mikataba na tulishapewa makisio ya kilo zinazotakiwa kuzalishwa’, alisema. Baada ya kutembelea kijiji hicho na kujionea uharibifu uliotokea, Mkuu wa Mkoa, Balozi Batida aliaahidi kuwasiliana na Mamlaka husika ya maafa ili kuangalia namna ya kuwasaidia. 

Aidha alielekeza Bodi ya Tumbaku, Chama Kikuu cha Ushirika wa wakulima wa tumbaku Mkoani hapa (WETCU LTD) na Afisa Ushirika kukaa na wahanga ili kuangalia namna ya kuokoa tumbaku iliyobaki. Katika ziara hiyo Balozi Batilda pia alitembelea wakulima wa kijiji cha Iyombakuzova katika kata ya Misheni na kujionea jinsi tumbaku ilivyostawi vizuri baada ya kutumia mbolea ya ruzuku iliyotolewa na serikali msimu huu. 

Alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na serikali ya awamu ya 6 kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima kwa kuwa itawasaidia kuboresha shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kuongeza mapato yao. Aliwahakikishia kuwa serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inajali sana wananchi hivyo itaendelea kuweka utaratibu mzuri wa upatikanaji pembejeo hizo ili kumaliza changamoto zilizopo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages