LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 28, 2023

MBUNGE MARIAM NYOKA AMTEMBELEA MWALIMU ALIYEJIFUNGUA WATOTO WANNE KWA MPIGO, AOMBA JAMII KUSAIDIA MALEZI

Na Muhidin Amri, Tunduru

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma (CCM) Mariam Nyoka, amemtembelea Mwalimu wa shule ya msingi Wenye Kata ya Nalasi Magharibi, Tunduru Judith Schalwe aliyejifungua watoto wanne kwa mpigo, Mei mwaka jana.


Mwalimu Judith Schalwe,anahitaji msaada wa hali na mali ili aweze kuwalea na kuwahudumia watoto wake watatu waliobaki baada ya mmoja kufariki dunia mwezi Septemba mwaka uliopita.


Akizungumza baada ya kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa Mwalimu Judith,Nyoka amewataka wadau na wananchi wenye uwezo kujitokeza kumsaidia mwalimu huyo ili aweze kuwalea watoto wake watatu.


Amesema licha ya Judith kuwa mtumishi wa umma,lakini  bado anakabiliwa na changamoto kubwa ya kimaisha,hivyo jamii inapaswa kumshika mkono kwa kumpa kile walichonacho kwa sababu  kazi ya kulea watoto watatu mapacha ni ngumu.


Nyoka, ametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwamo Pampasi,sabuni za kufulia na kuogea,unga wa mahindi,mafuta ya kupata,sukari,nguo na fedha taslimu  ambazo  zitatumika kumsaidia na kuwatunza watoto hao na amehaidi kumpa Pikipiki Mwalimu huyo  ili iweze kuwaingizia kipato.

Katika hatua nyingine Nyoka,ametoa msaada wa baiskeli ya magurudumu matatu kwa mkazi wa mtaa wa Mlingoti Magharibi Sophia Ali mwenye  ulemavu wa miguu.

Sophia Ali licha ya kuwa mlemavu anayehitaji msaada wa wasamaria wema,ni mama wa watoto saba kati ya hao watoto wanne ni walemavu ambao wanahitaji msaada wa hali na mali ili iweze kuwasaidia.

Kwa upande wake Mwalimu Judith,amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa kumpa ajira ya Ualimu Baba watoto wake Hamis Shaibu ambaye ana Diploma ya Ualimu, lakini hadi sasa hajapata kazi licha ya kutuma maombi mara kwa mara serikalini.

Amesema,anakabiliwa na hali ngumu ya maisha  kwani hata mshahara anaopata hautoshelezi kwa kuwa sehemu kubwa ya fedha  hizo zinatumika kwa ajili ya matunzo ya watoto wake.

Mwalimu Judith, ameshukuru Mbunge huyo kwenda kumuona na kumpa msaada wa vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto wake na kuwaomba wadau wengine kumsaidia.

Naye mume wa Judith Hamis Shaibu amemuomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,amsaidie kupata ajira ya kudumu ili  aweze kumsaidie mke wake kulea watoto wake hao, badala ya jukumu  hilo kumuachia mke pekee yake.

Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka akizungumza na mwalimu wa shule ya msingi Wenye Halmashauri ya wilaya Tunduru  Judith Schalwe ambaye alijifungua mapacha wanne mwezi Mei mwaka jana huku akiwa na watoto watatu kati ya wanne waliobaki Abiud Hamza, Hamis Hamza na Rose Hamza  baada ya  mmoja kufariki dunia mwezi Septemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages