Viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Kagera walimu wa shule za msingi na sekondari wakimsikiliza waziri Kairuki.
Na Lydia Lugakila Kagera
Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angella Kairuki amemuagiza Naibu katibu Mkuu (Elimu) TAMISEMI, Charles Msonde kuhakikisha mchakato ya posho mbalimbali za madaraka na posho nyingine za uongozi kuanza kulipwa kupitia akaunti benki ya kiongozi husika.
Waziri Kairuki ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kikao kazi cha tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa elimu na uwekaji wa mpango kazi wa utekelezaji kwa mwaka 2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Sido Rwamishenye manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Waziri Kairuki amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya viongozi wa elimu kwenye wilaya na katika maeneo mengine walimu wakuu wanapokuja kuidhinishiwa michakato ya vocha zao za malipo ya posho za madaraka na kupitisha saini zao mtu uhitaji apitishiwe pale fedha.
"Wapo wengine mpaka apatiwe sh. 20, 000 lakini wakati huo mtu ametoka labda wilaya ya Kyerwa, Ngara au Karagwe katumia fedha nyingi ikiwemo nauli kuja kufuata posho zake" alisema Waziri Kairuki.
Amemuelekeza Naibu katibu mkuu kuhakikisha suala la kulipa posho hizo kwa mchakato mrefu linakoma mara moja badala yake fedha hiyo ipite katika akaunti ya benki ya muhusika.
Amesema hategemei kuona mtu analetewa fedha pembeni kwenye akaunti alafu anaanza kuhamishwa kwa miamala jambo alilolitaja kuwa kujiletea matatizo ambapo watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha amesema kuwa lengo la kuweka mfumo huo mpya ni kutaka kupunguza urasmu, kuleta ufanisi na kuwapunguzia mzigo walimu kufuata fedha hizo kwa utaratibu wenye michakato mirefu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwalinda walimu hao ili wapate haki zao.
Waziri Kairuki ameahidi kuendelea kubadili mifumo mingine ambayo haiendi sawa katika sekta ya elimu.
Hata hivyo amepongeza Rais Dkt. Samia kwa kuendeleza na kuhakikisha posho hizo zinakuja kwa wakati.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇