Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe Albert John Chalamila akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake.
Na, Lydia Lugakila Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe, Albert John Chalamila ametaja kusikitishwa na tukio la Mwalimu Mkuu aliyeonekana akiwachapa viboko Wanafunzi kwa kuwakanyaga na kuwachapa miguuni hadi kuonekana wakichechemea kutokana na kosa la kutofanya kazi ya Nyumbani(Home Work) waliyopewa wakati wa likizo.
Rc Chalamila ametoa ufafanuzi wa tukio hilo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Januari 25, 2023.
Amesema kuwa kutokana na kuzunguka kwa Video katika mitandao mbali mbali ya Kijamii ameona ni vyema aombe radhi kwa Watanzania kutokana na tukio hilo ambalo linaumiza, kusisimua kadri lilivyoonekana.
Chalamila amesema tukio hilo limetokea Januari 10, 2023 ambapo Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi Kakanja iliyopo Kata ya Kakanja Wilayani Kyerwa Mkoani humo aitwaye Isaya Benjamin Emanuel aliyepiga viboko Wanafunzi zaidi ya mmoja huku upigaji wake ukileta taharuki kwa umma ya Watanzania.
Ameongeza kuwa katika video ile pia walionekana baadhi ya Walimu wa shule hiyo, waliokuwa wamekaa pembeni na kusikika wakicheka wakati Mwalimu Mkuu huyo akiwachapa wanafunzi hao sehemu ya miguuni.
Ameongeza kuwa kwa Mujibu wa Waraka wa Elimu no 24.wa mwaka 2002 kuhusu adhabu ya viboko, ni kuwa itazingatia ukubwa wa kosa, umri, jinsi,Afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja.
"Kosa la kwanza la Mwalimu Isaya alichapa viboko zaidi ya vinne kwa Kinyume na Waraka wa Elimu, adhabu ya viboko itatolewa na Mwalimu Mkuu au Mwalimu mwingine atakayeteuliwa na Mwalimu Mkuu kwa maandishi kila mara kosa linalostahili adhabu hii itakapotendeka" alisema Rc Chalamila.
Aidha, ameongeza kuwa Mwalimu Mkuu alistahili kwa kuwa ni mamlaka ya Nidhamu ya kuadhibu lakini upigaji wake umeonekana ni wa kuwakanyaga Wanafunzi miguu, kuwapiga kwenye miguu jambo ambalo lingeweza kupelekea afya zao kuwa na matatizo.
Amewataja Walimu walionekana wakifurahi wakati Mwalimu huyo akitenda tukio hilo kuwa ni wanne ambao ni Mwalimu Godson Rwabisho, Beatrice Osward Kaburakyage, James Josiah na Delphina Leonce ambao watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa Mujibu wa miongozo ya Elimu, Walimu ambao walitarajiwa kuwa walezi, washauri wa mkuu wa Shule lakini Kinyume chake wakaonekana kutofanya jukumu lao na kucheka ikiwa ni kukiuka jukumu la kuwa walezi na washauri wa Mwalimu Mkuu huyo.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa amesema Mamlaka yake ya nidhamu, chini ya Katibu Tawala wa Mkoa huo tayari hatua za kinidhamu zimechukuliwa ambapo Mwalimu Mkuu huyo amesimamishwa kazi na Kamati za uchunguzi zinaendelea kuchunguza uhalisia na vigezo vinavyostahili ili aweze kuchukuliwa hatua Stahiki ikiwa ni pamoja kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo Mkuu huyo Mkoa amemuagiza katibu Tawala Mkoani humo kuhakikisha anachukua hatua za kisheria kwa Mratibu Elimu Kata na kuchunguza zaidi kuhusu ufanisi wake na ubora wake katika utendaji kazi huku akiwasisitiza Wazazi, Walezi na Viongozi ngazi ya Kata kutembelea shule, kufanya vikao vya mara kwa mara na Wazazi pamoja na Walimu zaidi wabebe jukumu la kulea kwa Mujibu wa Kanuni na taratibu ya kazi zao.
Mdau, nakuomba uendelee kusikiliza/kuona kupitia clip hii ya video, Mwalimu Mkuu akiwasulubu kwa viboko wanafunzi ...
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇