Na Dismas Lyassa
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkombozi, Kata Pangani, Anasi Bwanari (wa kwanza kulia mwenye saa) akisikiliza jambo wakati viongozi wa CCM Kata walipotembelea shule ya Mkombozi.
MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Mkombozi, Kata Pangani, Halmashauri ya Mji Kibaha, Pwani ndugu Anasi Bwanari na wasaidizi wake pamoja na wananchi wa mtaa huo wamepongezwa kwa kushirikiana kuleta maendeleo katika eneo lao.
“Ukweli ni kwamba nimefurahishwa sana na taarifa hii ya kwamba wananchi kupitia Serikali yenu mmejenga shule hadi kufikia kwenye linta, kisha mkaomba msaada wa halmashauri kuezeka, ni jambo linalopaswa kutiliwa mfano,” alisema James Mgaya wakati wa ziara ya kamati ya siasa kutembelea shule mya ya msingi Mkombozi iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kusimamiwa na Serikali yao ya mtaa.
Nje ya ujenzi wa shule, hata vyoo na karo kubwa la kuhifadhi maji machafu kutoka chooni limejengwa kwa nguvu za wananchi chini ya usimamizi wa mwenyekiti na wasaidizi wake.
“Naomba sana mwenyekiti wa chama na mwenyekiti wa Serikali endeleeni kushirikiana na wananchi na wachama kuleta maendeleo katika mtaa wenu, hakika nimefurahishwa mno kuona nguvu kubwa sana za wananchi zimetumika kuleta maendeleo hapa,” alisema katibu wa CCM Kata Pangani, Masoud Seleman.
Mwenyekiti wa CCM Kata Pangani, Stanley Eliya aliuopongeza uongozi wa chama tawi la Mkombozi akisema kuwa kuonekana kwa maendeleo katika mtaa huo ni ishara kwamba viongozi wa chama wanasimamia vizuri Ilani ya CCM.
“Nakupongeza sana mwenyekiti wa CCM tawi la Mkombozi, ni ishara ya wazi kwamba unaisimamia vizuri Ilani, endeleeni kufanya kazi pamoja na Serikali, ni wazi mtafanikiwa kuleta maendeleo mengi” alisema Eliya.
Akizungumza kuhusiana na maendeleo katika mtaa huo mwenyekiti huyo (Anasi Bwanari) alisema anawapongeza sana wananchi wa Mkombozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kadri wanavyoombwa kujitolea.
“Shukrani za kipekee nazipeleka kwa wananchi wenzangu wa Mtaa wa Mkombozi, sisi tumekuwa na ushirikiano na ninaomba sana ushirikiano huu na kujitolea huku kuendelee, hata sasa tuko kwenye harakati za kuanza kujenga Zahanati ya mtaa,” alisema Bwanari.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇