LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 31, 2023

DISMAS LYASSA APONGEZWA KWA SHULE KUKAMILIKA, KESHO JUMATANO KUANZA UJENZI WA ZAHANATI YA MTAA

Dismas Lyassa, Mwandishi wa Habari na mtaalam wa Uongozi na Utawala ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mkombozi, Kata Pangani Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani akieleza namna gani walifanikiwa kujenga shule kwa nguvu za wananchi. Kesho jumatano wataanza rasmi ujenzi wa Zahanati

WANANCHI wa Mtaa wa Mkombozi, Kata Pangani katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Pwani wamempongeza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) tawi hilo ndugu Dismas LYASSA kwa  kuhamasisha vema maendeleo na kufanikisha kukamilika kwa ujenzi wa shule ya msingi kwa nguvu za wananchi. Kesho jumatano mtaa huo utaanza ujenzi wa Zahanati wakitumia pia nguvu za wananchi.
"Katika mtaa wetu hatukuwa na shule wala zahanati. Dismas alipohamia huku kuna wazee walimfuata na kumuomba agombee nafasi ya Uenyekiti wa tawi ili asadie maendeleo. Nae bila kusita alikubali. Mwanzo tulifikiri asingekubali kuwa kwenye nafasi hii kutokana na ukweli kwamba Dismas Lyassa sio kwamba amesoma nchi mbalimbali na ngazi mbalimbali zikiwamo Uandishi wa habari, pia Stastashahada ya Uzamili katika Uongozi na Utawala, lakini aliwahi kugombea Ubunge na kura za maoni kutotosha alipogombea huko Mlimba mwaka 2015. Tulihofia kuwa angeacha kutokana na umaarufu wake kwani huwa anaitwa pia hata kwenye televisheni mbalimbali kama mtaalam, hii nafasi inaonekana kama ndogo lakini alituahidi atashirikiana na sisi hadi mtaa wetu uwe na mabadiliko, tunashukuru tunayaona mabadiliko, hatukuwa na umeme, aliweza kupigania na kutoa msukumo, sasa tuna umeme, hatukuwa na shule sasa tuna shule na watoto wanaanza masomo rasmi hivi karibuni, lakini ni faraja pia kwamba kesho jumatano ujenzi rasmi wa zahanati unaanza," anasema Jacqueline Mrina, mkazi wa mtaa huo akipongeza maendeleo katika mtaa huo.
Wananchi wengine wanasema siri ya kufanikiwa huko ni Dismas Lyassa kuhamasisha harakati za maendeleo wananchi na wanachama na wakati fulani kuwabeba viongozi wa Serikali ya mtaa na mabalozi kuwapeleka nje ya mkoa kwa ajili ya kupata mafunzo ya uongozi.
"Kwa kweli tunampongeza sana Dismas Lyassa, ni mwenyekiti pekee wa tawi katika kata ya Pangani na pengine wilaya nzima au mkoa mzima wa Pwani ambaye mara baada ya kuingia madarakani  katika uchaguzi wa mwaka jana aliwachukua viongozi wote wa tawi lake wakiwamo mabalozi na wale wa Serikali ya mtaa na kuwapeleka Morogoro ambako walinolewa kwa kupewa elimu kuhusu masuala ya uongozi na namna ya kuleta tija katika uongozi," alisema James Mgaya, Katibu Mwenezi CCM Kata Pangani akimzungumzia Dismas Lyassa.
Aidha Mwenyekiti wa CCM Kata ya Pangani, Stanley Betram, alimpongeza pia Dismas Lyassa na kumuahidi ushirikiano katika tawi lake na maendeleo yote kwa ujumla.
"Nimeagiza kamati nzima ya siasa kata Pangani kesho jumatano kwenda Mkombozi kuungana na Dismas Lyassa na viongozi wake katika kuanza ujenzi wa Zahanati hii mpya inayojengwa kwa nguvu za wananchi," anasema Betram.
Mtaa wa Mkombozi hauna Zahanati, hivyo ujenzi huo utawasaidia sana wananchi kupata huduma za afya ambazo kwa sasa wanalazimika kuzifuata katika mitaa mingine.
"Ni kweli niligombea Ubunge Jimbo la Mlimba mwaka 2015 kura za maoni hazikutosha, baadae niligombea pia Ubunge wa Afrika Mashariki kura hazikutosha. Nikiwa hapa nyumbani kuna wazee walinifuata kuniomba nigombee Uongozi wa tawi, nilitafakari na familia na kukubaliana na nafasi hiyo hasa baada ya kubaini kwamba kuna msaada ambao naweza kuutoa kwa kushirikiana na wana CCM na wananchi wenzangu, nilikumbuka pia baadhi ya watu waliosoma zaidi yangu na wenye uzoefu zaidi yangu ambao waliwahi kuwa na nafasi kama hizi au hata za chini zaidi. Kwamba, azma yangu ni kuleta mabadiliko, niliona hili ni jukwaa pia la kushirikiana na wananchi wenzangu kuleta maendeleo.
"Hapa kwetu ambacho nilikifanya ni kwamba tuliandaa Ilani ya Mtaa, niliiwasilisha kwenye kamati ya siasa wakaibariki... kisha tulikaa na wagombea na kukubaliana na kuwakabidhi Ilani nje ya ile Ilani kuu...kwa hiyo viongozi wa Serikali ya Mtaa wana wajibu wa kujibu maswali ya namna gani wametekeleza Ilani ya CCM tawi ambayo ilitengenezwa kulingana na mahitaji ya eneo, pia wanalo jukumu la kuitekeleza ile Ilani kuu ambayo kimsingi haina tofauti, isipokuwa tuliona tuandae Ilani maalum ya tawi ili wajibu kwa kina nini katika mtaa wanapaswa kuzingatia.
"Mbinu nyingine za kupata mafanikio ni uwazi, hapa mtaa kwetu chama tumetenga siku maalum ya wananchi na wanachama kuja ofisini kubadilishana mawazo juu ya namna ya kuimarisha maendeleo kwenye eneo letu, kuleta malalamiko au chochote wanachotaka. Fedha zote zinazokusanywa kutoka kwa wanachi, chama kimeagiza ni lazima zitolewe lisiti na pia majina ni lazima yabandikwe hadharani nje ya ofisi ya Serikali ya mtaa, kutofanya hivyo tumekubaliana kuwaita viongiozi wa mtaa katika kamati za maadili ikiwamo kuchukua hatua nyingine zozote zinazowastahili. Kwa bahati nzuri Serikali imekuwa sikivu, hatujawahi kuwaita kamati ya maadili, tunafanya kwa karibu sana, tunafahamu kila kinachoendelea katika Serikali.
"Jamii tunaisisitizia kuhoji bila woga pale wanapoona mambo fulani hayaendi sawa, kwamba chama kitawalinda, hii imesaidia wananchi sio tu wanakipenda zaidi chama cha mapinduzi, lakini pia wanakuwa wazi kutoa mawazo au hata kuonya au kushauri bila woga," anasema Dismas Lyassa ambaye ni mhitimu wa Stashahada ya Uzamili katika Uongozi na Utawala kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Aprili 2014.
"Wapo marafiki zangu ninapowaambia mimi ni mwenyekiti wa CCM tawi, huwa wananishangaa na wengine kunidhihaki, lakini katika maisha fanya unachokiona unakipenda au kinafaa, usiangalie sana watu wanasema mimi....kila mtu anapaswa kuishi maisha yake, sio ya wengine," anasema Dismas Lyassa.
"Msingi wa kufanikiwa kwetu ni hamasa, uongozi ni uwezo wa kushawishi/kuhamasisha na kufanya mambo unayotaka yatokee... hiki ndicho kimesababisha haya yote...nawashukuru sana wananchi wenzangu kwa kunielewa...na kukubaliana kushirikiana," anasema.

Leo mafundi wakilipima eneo kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Mtaa wa Mkombozi 

Baadhi ya matofali yakishushwa leo tayari kwa ajili ya kuanza ujenzi kesho

Baadhi ya wananchi wa Mkombozi wakiwa katika mkutano wa kujadili kuhusu ujenzi leo. Ujenzi wa Zahanati unaanzisha kesho jumatano

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages