Sehemu ya vijana wakifuatilia mafunzo hayo.
Mfadhili wa mafunzo hayo Mwemezi Ngemera akiweka msisitizo kwa vijana juu ya kuzifikia ndoto zao.
Na Lydia Lugakila,
Kagera.
Jumla ya vijana 70 kutoka shule za sekondari na msingi katika kata za Kanyigo na Kashenyi wilayani Misenyi mkoani Kagera ambao ni kati ya umri wa miaka 12- 18 wamenufaika na elimu ya kuwajengea uwezo juu ya kufuata ndoto zao wakiwa katika umri mdogo ili wajitambue na kufikia malengo yao.
Akiendesha semina hiyo iliyofanyika katika shule ya sekondari Kanyigo Doreen Ngemera mwenye umri wa miaka 17 mwanafunzi wa kidato cha tano amesema kuwa wameamua kuwajengea uwezo vijana hao ili kufuata ndoto zao wakiwa katika umri mdogo kwa kuwafanya watambue ndoto zao mapema jambo litakalo wasaidia kuweka bidii ili watimize ndoto hizo bila vikwazo.
Doreen amesema vijana wengi wana uwezo mkubwa ila bado hawajatambua waanze wapi ili kufikia ndoto zao zitakazo wasaidia kwa maisha ya baadae.
"Mimi ni kijana mdogo nina umri wa miaka 17 nimeona niwalete pamoja vijana hawa wapate elimu ya kutambua ndoto zao na kuzifanyia kazi wakiwa wadogo ili kwa baadae wasiwe wategemezi katika familia zao" alisema Doreen.
Ameongeza kuwa kwa mwaka 2021 walifanya semina ya namna hiyo ya utambuzi wa vipaji walivyonavyo vijana ambapo waliwafikia vijana 100 na hadi sasa wametambuliwa na wengine kupata fursa mbali mbali huku akiwaomba wazazi kutokuwa sehemu ya kukatisha ndoto za vijana hao.
Aidha kwa upande wake mfadhili wa semina hiyo Bwana Mwemezi Ngemera amesema wamelenga kundi la vijana ili kuwanoa kabla ya kuelekea uzeeni na kuwa baada ya kugundua baadhi ya wazazi kutokaa na kuwasikiliza vijana wao katika kutambua na kutimiza ndoto zao wameamua kuja na muarobini huo wa kuwanoa.
Ngemera amempongeza Doreen kwa kuwaleta pamoja vijana hao ambapo amewahimiza wazazi kutambua majukumu yao kwa watoto ikiwa ni pamoja na kutowakatisha tamaa katika kufikia malengo yao huku akiahidi kutenga muda mzuri kuwakutanisha vijana hao katika awamu ijayo ili kuwa na wasomi wengi kwa baadae.
Naye mgeni rasmi katika semina hiyo ambaye ni mchungaji kutoka Kanisa la kiinjili la Kilutheli Tanzania KKKT dayosisi ya kaskazini Magharibi Joas Kahesi amesema kuwa vijana wasipotambua ndoto zao wakiwa wadogo mbeleni kuna shida.
"Kujitambua kunatokana na kuwa na mtizamo chanya na kutokatishwa tamaa jijengeeni msingi wa kuacha uvivu jamii haihitaji vijana wawe mzigo kwa baadae, hivyo ni lazima kila kijana awe na matamanio akiwa na umri mdogo kwa kutunza ndoto yake"alisema mtumishi wa Mungu.
Hata hiyo Maraika Gedi,Shafiu Faki na Fatiha Yunus ni moja kati ya wanufaika wa mafunzo hayo wamepongeza wawezeshaji na kukiri kupata uelewa kwani wamejua namna ya kutotegemea ndoto moja, kufuata ndoto zao, kujiamini, huku wakiahidi kuwa mabalozi kwa vijana wenzao na pia kuwaomba wazazi kujenga utamaduni wa kuwaruhusu watoto kushiriki mafunzo mbalimbali yanapotolewa na wafadhili mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇