Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika Yanga imefuzu hatua ya makundi kwenye michuano hiyo baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Club Africain amvayo ilikuwa mwenyeji wa Yanga katika mchezo uliopigwa jana ilikubali kulala kwa bao 1-0, bao lililofungwa na kiungo mtaalamu Aziz Ki baada ya kupokea pasi nzuri na straika, Fiston Mayele dakika 79.
Ki ambaye aliingia kipindi cha pili alionekana kuongeza umakini kwa Yanga haswa eneo la kushambulia hadi kupata bao lililoibua ushindi huo.
Kutokana na kikosi cha Yanga kilivyoaanza, walikuwa wakicheza zaidi kwa nidhamu kwenye maeneo yote hadi kuwabana Club Africain kushindwa kupata hata bao la kuotea.
Pengine matokeo hayo yamekuwa na faida na furaha kwa Yanga kutokana na kupata nafasi ya kwenda hatua ya makundi kwenye michuano hiyo.
Inaelezwa wachezaji wa Yanga baada ya kutinga hatua ya makundi mifuko yao itajazwa minoti baada ya kupewa ahadi si chini ya Sh200 milioni kama bonansi ya ushindi.
Yanga inatinga hatua ya makundi kwenye kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuomdolewa Ligi ya mabingwa Afrika na miamba ya soka ya Sudan, Al Hilal.
Mechi ya kwanza Yanga ikiwa nyumbani dhidi ya Club Africain ilitoka suluhu Uwanja Benjamin Mkapa na imekwenda kupata matokeo ya ushindi Tunisia.
YANGA KUJAZWA MANOTI
Yanga baada ya kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika itapata Dola za Kimarekani 275,000 zaidi ya Sh 500 milioni.
Yanga itapata mkwanja huo kutoka Shirikisho la soka Afrika (CAF) kama pesa ya sehemu ya maandalizi baada ya kutinga hatua ya makundi.
Yanga inaenda hatua ya makundi ya mashindano hayo baada ya kufanya hivyo mara ya mwisho 2018.
#Mwananchi Digital
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇