LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 13, 2022

TEMEKE KUFANYA USAFI FUKWE ZOTE WIKENDI YA JUMAMOSI NOVEMBA 19, 2022

Na Christopher Lissa, UPL
Wadau wa usafi  wa mazingira  wametakiwa kujitokeza kushiriki   usafishaji wa  fukwe  wilayani Temeke baada ya fukwe hizo kutokusafishwa kwa kipindi kirefu.

Mwito huo umetolewa na  Mratibu wa  Kampeni ya Safisha Pendesha Dar es Salaam, wilayani Temeke, Asya  Mbarouk, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hili,  Dar es Salaam,   kuhusu kampeni  ya  Kurasini Beach Clean Up, inayotarajiwa kufanyika Novemba  19 mwaka huu.

Asya, alisema kampeniF hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Tanzania Cleanup and Conservation Initiative (TCCI) kwa kushirikiana na  Wadau wa Usafi wa Mazingira Temeke (WAUMATE).

“Mgeni Rasmi atakuwa ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,  Arnaold Peter. Usafi utafanyika katika Kijiji cha Wavuvi Kurasini. Wadau tunaomba wajitokeze kushiriki,”alisema Asya.

Asya alisema, huo ni mwendelezo wa Kampeni ya Safisha, Pendesha Dar es Salaam, iliyoasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.

Awali  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya  TCCI,   Kingungo Salum, alisema  itakuwa  ni mara ya  kwanza kwa kampeni kubwa ya usafi kufanyika katika fukwe  za  Wilaya ya  Temeke  kupitia taasisi  za mazingira,wadau na wananchi.

Alisema kampeni hiyo ya kusafisha fukwe itakuwa endelevu kwa fukwe zote  wilayani humo.
“Napenda kuwasisitiza wadau na taasisi zingine kushiriki ili kuifanya Temeke yetu iwe safi na salama. Pia watu  binafsi na vikundi  waje kushirikiana na  WAUMATE  kufanya usafi huo,”alieleza Salum.

Baadhi ya wadau wa usafi  wilayani humo, wamepongeza hatua hiyo  ili fukwe hizo  ziwe kivutio  na mahali salama  kwa wananchi kupumzika au kufanya shughuli zao.

Hivi karibuni Idara ya Mazingira wilayani Temeke, ilifanya kampeni kubwa ya usafi katika eneo la Mbagala Rangi Tatu, katika Kata ya Kibonde Maji, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo na Meya wa Manispaa hiyo, Abdallah Mtinika.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makalla alielekeza kila ifikapo Jumamosi ya  mwisho wa mwezi kuwa siku ya usafi, mkoani humo.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages