Na Alfred Lasteck
BBC
Fiston Mayele, mshambuliaji raia wa DRC amekua kiungo muhimu kwa klabu ya yanga
Klabu ya Yanga ya nchini Tanzania imeandika rekodi mpya ya kucheza mechi mfululizo za Ligi Kuu nchini humo bila kupoteza, ikifikisha michezo 49,rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na klabu nyingine yoyote kwenye historia ya soka katika nchi hiyo mwanachama wa Afrika Mashariki.
Rekodi kama hii imewahi kuwekwa na Klabu ya Arsenal katika msimu wa 2003/04. Rekodi ambayo inabaki kwenye kumbukumbu za mashabiki wa soka ulimwenguni haswa wale wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Aidha Kwa Tanzania, rekodi ya Yanga inakuja baada ya Jumamosi kuifumua Mbeya City kwa mabao 2-0 katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Mara ya mwisho kwa Yanga kupoteza mechi kabla ya kuandika rekodi hii ni Aprili 25, mwaka jana ilipolala kwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.
Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli katika moja ya mechi zao
'Rekodi za kibabe'
Kwenye mechi hizo 49 za Ligi Kuu, Yanga SC imefanikiwa kufunga magoli 83, wakiruhusu magoli 16 na kutoka bila kuruhusu bao lolote langoni michezo 34, huku golikipa Djigui Diarra akiwa kinara wa 'Cleansheet' msimu uliopita (15).
Katika kipindi chote hicho Yanga imefanikiwa kushinda michezo 39 na kutoka sare michezo 10, huku ikifanikiwa kubeba mataji manne, ligi kuu mara moja, Kombe la Shirikisho nchini Tanzania mara moja na Ngao ya jamii mara mbili.
Yanga ni miongoni mwa klabu yenye idadi ya mashabiki wengi Afrika mashariki
Yavunja rekodi ya Azam FC
Yanga iliyo chini ya Kocha raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi imepata matokeo ya ushindi na sare tu. Kabla ya Yanga kuweka rekodi hiyo mpya nchini Tanzania, timu ya Azam ndio iliyokuwa ikiishikilia rekodi ya kucheza mechi 38 bila kupoteza, rekodi iliyodumu kwa muda wa miaka saba ambayo ni sawa na siku 2856 kabla ya vijana wa Yanga ‘Jangwani’ kuivunja msimu huu na kuandika rekodi yake mpya.
Yanga ilifikia rekodi ya Azam msimu huu Agosti 16 baada ya kuifunga Polisi Tanzania kwa mabao 2-1.
Msimu wa 2022/21 Yanga haikupoteza michezo saba ya mwisho wa msimu, ikacheza na kutwaa ubingwa bila kupoteza msimu mzima wa 2021/22 na mpaka sasa kwenye michezo 12 ya msimu huu unaoendelea wa 2022/23.
Klabu hii ina wachezaji wazawa wa Tanzania na maeneo mbalimbali ya bara la Afrika
Yanga, Azam zabebana kutengeneza rekodi za 'haraka'
Ukirejea rekodi ya Azam utabaini ilitokana na kipigo kutoka kwa Yanga, iliyowachapa bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Februari 23, 2012 na hivyo Azam kukaza buti na kuzitimiza mechi hizo 38 kabla ya Klabu ya JKT Ruvu (sasa JKT Tanzania) kuwatibulia rekodi hiyo Oktoba 25, 2014 ikiwa zaidi ya siku 900 bila ya kuonja machungu ya kipigo.
Ukirejea kwa Yanga, imetumia muda mfupi zaidi kuifikia na kuivunja rekodi hiyo ya Azam na kuiboresha zaidi ikitumia jumla ya siku takribani 500 tu. Kama umesahau ni kwamba ni Azam hao hao ndio walioipa akili Yanga kukaza buti kwenye mechi hizo.
Yanga ilipoteza mechi ya mwisho mbele ya Azam Aprili 25, 2021 na baada ya hapo wababe hao wamekuwa wakitoa vipigo ama kuambulia sare na kuweka historia hadi sasa.
Rekodi za Yanga kwa Tanzania
Yapo mambo mengi ya kusisimua yaliofanywa na klabu hiyo tangu ianzishwe mwaka 1935, kubwa zaidi ndio kinara wa mataji ya ligi kuu Bara, ambapo wamechukua mara 28, wakiwaacha mbali watani wao Simba ambao wana 22.
Rekodi za Afrika zikoje?
Miongoni mwa vigogo wa Afrika ambao wanashikilia rekodi ya kucheza michezo mingi hususani ya ligi bila kupoteza ni pamoja na hawa;
Klabu ya Asec Mimosas ilicheza michezo 108 bila kupoteza tokea mwaka 1989 mpaka 1994.
Esperance de Tunis walicheza michezo 85 bila kupoteza kwenye ligi kuu Tunisia tokea mwaka 1997 mpaka mwaka 2001 ambapo walipokonywa ushindi mechi ya 86 baada ya kuvunja kanuni ya kumchezesha mchezaji asiyeruhusiwa kwenye ushindi wao wa magoli 6 dhidi ya Dejrba
Al Ahly ya Misri wao pia wanashikilia rekodi ya kucheza michezo 45 ya ligi ambapo, rekodi ilivunjwa na mchezaji wao wa zamani John Antwi ambapo wakati huo alikuwa anaitumikia Misr El Maqsa.
Rekodi za Afrika mashariki
Klabu ya Gor Mahia ya Kenya ni miongoni mwa klabu zenye rekodi kubwa ya kutopoteza mchezo ambapo ilimaliza mechi zaidi ya 20 katika misimu ya 1976 na 2015. Sambamba klabu hiyo, Klabu ya APR ya Rwanda, KCCA ya Uganda ni miongoni mwa timu zenye rekodi ya kucheza michezo mingi bila ya kupoteza.
Je rekodi ya Yanga na Arsenal zikoje?
Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania wameingia kwenye anga ya Arsenal kwa kufikisha mechi 49 bila kupoteza mechi huku wakiwa wameshinda michezo 39.
Rekodi ya Arsenal ilianzia Mei 2003 kwenye ushindi wa magoli 6-1 kwenye uwanja wa HighBury na kudumu na rekodi hiyo mpaka Oktoba 2004 ambapo utepe ulikatwa katika Uwanja wa Old Trafford walipofungwa mabao 2-0 na Manchester United, magoli ya washambuliaji Rud Van Nestelrooy na Wayne Rooney. Katika kipindi hicho Arsenal walicheza mechi 49 huku wakishinda michezo 24 tu.
Usiyoyajua kuhusu Yanga
Mwaka 1968 Yanga ndiyo ilikuwa klabu ya kwanza kupata ushindi wa mabao mengi zaidi kwa kuwafunga wapinzani wao Simba mbao 5-0 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Maulid Dilunga na Saleh Zimbwe waliofunga mawili kila moja na lingine la Kitwana Manara ‘Popat’.
Mwaka 1969/70 Yanga iliingia katika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali kwa miaka miwili mfululizo katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika).
Mwaka 1998, mabingwa hao waliingia katika rekodi nyingine kwa kufanikiwa kuwa klabu ya kwanza kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Rekodi hiyo imevunjwa kwa kishindo na Simba mwaka 2003 walipofanikiwa kutinga hatua hiyo kwa kuing’oa walikuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri.
1993/99- Ni mwaka ambao Yanga iliingia katika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati nje ya ardhi ya Tanzania, ambapo ilitwaa nchini Uganda misimu miwili mfululizo kwa kuifunga SC Villa katika fainali hizo mbili tofauti. Kwa upande wa Tanzania, Simba ndiye kinara ametwaa mara sita akifuatiwa na Yanga mara tano.
Mafanikio ya kimataifa bado mtihani kwa Yanga
Mbali na klabu hii kuwa imara katika ligi ya nyumbani, lakini bado imekua ikiwanyima raha za kimataifa mashabiki zake. Mara kadhaa imeshiriki kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho lakini imeshindwa kuandika historia mpya.
Yanga ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 toka kwa mabingwa wa Sudan Al Hilal katika mchezo wa marudiano hatua ya 32.
Imani ya mashabiki wa klabu hiyo sasa imebaki katika Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya yanga kufuzu hatua ya makundi kwa kupata ushindi jumla ya bao 1-0 dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Je itafanikiwa? ni jambo la kusubiri.
KUHUSU KLABU YA YANGA
Ilianzishwa mwaka 1935
Makao Makuu- Dar es Salaam, Tanzania
Rais wa Klabu- Hersi Said (Tanzania)
Kocha Mkuu - Nasreddine Nabi (Tunisia)
Nahodha - Bakari Mwamnyeto (Tanzania)
Mfungaji Bora wa muda wote - Mohammed Hussein 'Mmachinga'(Tanzania)
Mfungaji kinara kwa sasa- Fiston Mayele (DRC)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇