LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 28, 2022

RC SERUKAMBA AWASHUKURU IRAMBA KWA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA KATIKA KUINUA KILIMO NCHINI

Na Hemed Munga, Iramba, Singida
Mkuu wa mkoa wa Singida Peter Serukamba amewashukuru wananchi wa Iramba kwa kutekeleza kwa kivitendo juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua na kuthamini mchango wa kilimo katika Taifa la Tanzania.

Serukamba ametoa pongezi hizo juzi Septemba 26, 2022 baada ya kufungua kongamano la uzinduzi wa Msimu wa Kilimo 2022/2023 katika Uwanja wa ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba mjini hapa.

Alisema kuwa kushiriki kwa wakulima na wananchi mbalimbali kumekua chachu ya wao kuonesha nia ya dhati ya kuunganisha mnyororo na kuleta mageuzi katika kilimo na ufugaji.

Aidha, aliongeza kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Rais Samia ambaye amejitoa kwa dhati kwa ajili ya kulitumika Taifa hili kivitendo.

‘’ Ndugu wakulima naomba mfahamu kuwa Rais wetu mpendwa amejitoa kwa dhati kwa kuongeza bajeti ya kulimo kutoka Tsh 294 bilioni hadi Tsh 751.1 sawa na ungezeko la asilimia 155.34.’’ alisema RC Serukamba

Aidha, alifafanua kuwa fedha hizo zitaimarisha utafiti, upimaji wa udongo, masoko ya kilimo, kuimarisha huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, kutoa ruzuku ya mbolea, kuboresha na kuimarisha miundombinu ya hifadhi ya mazao katika msimu huu wa kilimo 2022/2023.’’

Alibainisha kuwa serikali imejipanga kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wote waliojiandikisha katika mfumo maalumu, hivyo kila alie jiandindikisha atapata mbolea.

Aliongeza kuwa Serikali ya Rais Samia imepenguza bei ya mbolea ili kuwawezesha watanzania kupata mbolea hiyo.

‘’ Kwa kweli tunakila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa kupunguza bei ya mfuko wa mbolea ya Yurea mfuko wa kilo hamsini kuuzwa kwa Tsh 70,000 toka kwenye bei ya sasa Tsh 124,734, DAP Tsh 70,000 toka kwenye bei ya sasa 131,676, NPK kuuzwa Tsh 70,000 toka bei ya sasa 122,695, huku mbolea ya KANI kuuzwa Tsh 60,000 kutoka bei ya sasa 108,156 na mbolea ya SA kuuzwa Tsh 50,000 toka bei ya sasa Tsh 82,852.

Aidha, alisema ni mara ya kwanza kwa nchi ya Tanzania tangu kupatikana kwa uhuru kuingiza mbolea sokoni inayozalishwa katika jiji la Dodoma.

‘’ Tutaingiza sokoni mbolea mpya inayoitwa FOMI OTESHA ambayo inatengezwa jijini Dodoma nakuuzwa kwa mfuko wa kilogramu 25 sh 35, 000’’

Ni mbolea ambayo inatengezwa kwa malighafi za asili pamoja na kemikali hivyo kuifanya ardhi ya watanzania kutokufa na kukuza mazao ya watanzania.

‘’ Kwa kweli ninampongeza sana Rais Samia kwa sababu ameanza kwa vitendo safari ndefu, kubwa na nzuri ya mapinduzi ya kijani, hivyo ninaomba tumuunge mkono kwa kufanya kazi kwa bidii mashambani huku tukitumia ruzuku hii ya mbolea.’’

Katika hatua nyingine, RC Serukamba amewataka Wadu wote wakilimo kuwa mfano bora wa kutoa elimu na kulima mazao ya biashara yanayopatikana wilayani hapa.

‘’ Sina shaka kuwa wadau wote mlioshiriki hapa mtahusika katika ukuzaji wa kilimo kivitendo. Aidha niwaombe wadau wote kuwa na mikakati ya kukuza kilimo na ifikapo mwisho wa msimu huu mnipatie taarifa ya tathimini kwa kiwango gani mmekuza kilimo Iramba na Mkoani Singida.’’

Akitoa taarifa ya mafaniko ya Kongamano la kilimo lililofanyika mwaka jana, Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleimani Mwenda alisema kuwa wakulima walipata mkopo wa trekta 15 zenye thamani ya Tsh 5.4 milioni ukilinganisha na kabla ya kongamano hilo ambapo NMB benki walikuwa wakikopesha trekta 4.

Pia, kwa upande wa pawatira walikopesha 28 huku mikopo ya wajasiriamali 22 yenye thamani ya Tsh 200 milioni.

Aidha, Aliomuomba mkuu huyo wa mkoa wa Singida kufikisha salamu kwa Rais Samia ambaye amatoa pikipiki 20 kwa maafisa Ugani na kuipa wilaya ya Iramba Tsh 8 bilioni kwa ajili ya kufanya matengenezo na maboresho ya skimu ya umwagiliaji kijiji cha Masimba wilaya hapo.

‘’ Tunaamni uzalishaji kwa msimu huu utakuwa mkubwa, hivyo tufikishie salamu kwa Rais Samia kwa kuteletea fedha hizi nasi tunaahidi kuwa tutazisimamia ili zilete tija.’’

Wakiongea na mwandishi wetu wakulima toka katika wilaya hiyo walionesha Imani ya mafaniko makubwa katika msimu wakilimo ujao kwa sababu serikali imewajali kwa kuwaletea mbolea ya ruzuku kwa wakati.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama kikuu cha Ushirikia Mkoa wa Singida, (SIFAKU) Yahaya Hamisi aliishukuru serikali kwa kuwapunguzia mbolea ya zuruku, hivyo aliwashauri wakulima wenzake kulima kwa kufuata taratibu na kanuni za ulimaji ili wapate tija.

Naye Simioni Msengi aliiomba serikali na wadau kuwahisha upatikanaji wa pembejeo kabla ya msimu kuanza ili kurahisisha upatikanaji.

Kufanyika kwa kongamano hili kunafanya kuwa ni kongamano la pili kufanyika katika wilaya hiyo huku mafanikio yakiwa ni mengi kwa wakulima na wadau wa kilimo.

Mkuu wa mkoa wa Singida Peter Serukamba akimsikiliza Mkulima aliyekuwa akionyesha mazao ya kilimo, wakati alipofungua Kongamano la Uzinduzi wa Msimu wa Kilimo 2022/2023 katika Uwanja wa ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba juzi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleyman Mwenda.

Mkuu wa mkoa wa Singida Peter Serukamba akifungua Kongamano la Uzinduzi wa Msimu wa Kilimo 2022/2023 katika Uwanja wa ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba kwa kuendesha trekta lililopatikana baada ya Kongamano liliofanyika msimu wa kilimo 2021/2022. (Picha na Hemedi Munga)


 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages