Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akifurahia jambo kutoka kwa Mwenyekiti Bi. Fatma Mgonja wa Shina namba 2, tawi la Msasani kata ya Kaloleni, Wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua mradi uboreshaji vibanda vya biashara wa Chama Old Moshi ikiwa sehemu ya ziara yake ya Chama pamoja na kukagua, kuhimiza na kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025.
Wafanyabishara wa samaki waliondolewa katika soko la Manyema kwenda Pasua Manispaa ya Moshi wamemlilia katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo wakitaka warejeshwe soko lao la awali.
Wakizungumza leo jumatano Agusti 3, 2022, huku wakitokwa na machozi katika eneo la Old CCM ambako katibu mkuu alifika kuangalia mradi wa ujenzi nyumba za biashara za chama hicho, wananchi hao wamedai kuwa wananyanyasika na bidhaa zao na kutesrka kwa kuwa soko walilotakiwa kwenda halifai kwa biashara.
Wafanyabiashara wa samaki wabichi, walitakiwa kuondoka katika soko la Manyema kuanzia Machi mosi mwaka huu, na kuhamia soko la Pasua smbako kumejengwa miundombinu, jambo ambalo wafanyabiashara hao walipinga wakidsi hakuna biashara.
Wakati Katibu Mkuu akizungumza na maelfu ya wananchi ambao wamejitokeza katika eneo hilo, wakina mama watatu ambao ni sehemu ya wafanyabiashara hao, walipiga magoti mbele ya gari yake huku wakiangua kilio, hali ambayo ilimlazimu katibu mkuu kuacha kuzungumza na kuagiza wapewe kipaza sauti, ili waweze kuzungumza.
Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara hao amesema wamefukuzwa katika soko la Manyema wakidaiwa kufanyia biashara barabarani na kupelekwa soko la Pasua ambako hapafai kwa ajili ya biashara zao.
“Baba sisi tunateseka hapa Moshi, katika soko la Manyema tumefukuzwa tukiambiwa tuko barabarani, lakini tulikuwa eneo sahihi, tumefukuzwa bila sababu, tunaomba msaada wako baba, tunateseka sana”amesema mmoja wa wakina mama hao.
Baada ya kauli ya mama huyo, Katibu mkuu amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Moshi Abas Kayanda kutoa maelezo kuhusiana na malalamiko ya wananchi hao, ambapo amesema Manispaa ya Moshi kwa kutumia mapato yake ya ndani ilitenga fedha Sh 250Milioni kwa ajili ya kukarabati soko la Pasua ili liweze kutumika kwa ajili ya biashara ya samaki.
“Sehemu ambayo wanaisema ambayo walikuwa wakifanyia biashara ni eneo la chini ambako hakuna miundombinu na kiafya si salama, hivyo kupitia vikao vya madiwani na vikao vingine viliidhinisha fedha Sh 250Milioni kwa ajili ya kukarabati soko la Pasua, ili wafanyabiashara hao waweze kufanya biashara katika maeneo salama”.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Wilaya imeonekana kutoungwa mkono na mamia ya wananchi waliokuwa katika eneo hilo ambao walipiga kekele wakidai kuwa walifukuzwa bila kushirikishwa na kupelekwa eneo ambalo halifai kwa biashara.
“Eneo hilo linafaa kutengenezwa kuwa la kisasa na kufaa kwa biashara?alihoji katibu mkuu ambapo wananchi waliitika kwa sauti kuwa linafaa huku mkuu wa Wilaya naye akisema zikipatikana fedha ikajengwa miundombinu, patafaa kwa biashara.
Akizungumza Katibu Mkuu Chongolo, alitoa siku saba kwa wataalamu wa Manispaa ya moshi chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo kufanya tathimini na kuandaa michoro, ili kuona zitahitajika fedha shilingi ngapi ili kuweza kukarabati soko la manyema na kumfikishia taarifa.
“Mkuu wa Wilaya, wewe ndiye kamisaa wangu, simamia ndani ya wiki moja, wataalamu wafanye tathimini ya hilo eneo, kama linafaa kwa ajili ya biashara, wachore michoro kwa ajili ya miundombinu ya soko hilo, baada ya wiki moja nategemea taarifa itakuwa imekamilika na utaniletea ili sisi tusaidie kusukuma hiyo fedha ya kujenga soko katika eneo hilo la Manyema”. Amesema Chongolo
Katibu mkuu Chongolo yupo katika ziara ya kikazi ya siku tano Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo kwa leo yupo Moshi Mjini na Moshi vijijini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇