WANANCHI wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro wamehakikishiwa utatuzi wa changamoto ya barabara kwa ujenzi wa kiwango cha Lami cha kutoka Bomang’ombe, Chekimaji-TPC yenye urefu wa Kilometa 25.7 inayounganisha vijiji mbalimbali na kuondoa kero ya changamoto ya usafiri na vumbi kwa wakazi hao.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 2 Agosti, 2022 na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo mara baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Chekimaji na nyumba za watumishi katika Kata ya Masama Rundugai wilayani Hai,kinachojengwa na serikali,halmashauri na nguvu za wananchi kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 600.
Chongolo alisema kilio cha wananchi wa Hai na kata mbalimbali za wilaya hiyo ambazo barabara hiyo ya mchepuko ya vumbi inawaunganisha kurahisisha usafiri wameomba mara kadhaa barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami kwani hivi sasa imekuwa kero kwao kutokana na ubovu na vumbi.
“Hili la barabara nalichukua, hii barabara itajengwa kwa kiwango cha lami, naichukua kwa uzito na Rais Samia Suluhu Hassan ameitamka kwa uzito, ni barabara ya mchepuko itarahisisha na kupunguza msongamano,”alisema Chongolo.
Chongolo amesema kazi ya serikali ni kutafuta njia ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuwa kero hiyo ya barabara itatatuliwa ili wananchi wapate maendeleo.
Amesema barabara hiyo ikijengwa kwa lami inafungua uchumi wa Moshi na Hai na kwa kuweka vitega uchumi lakini pia inarahisisha na kuounguza msongamano kwenye barabara kuu ya Moshi -Arusha.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo cha Afya cha Chekimaji na nyumba za watumishi vinavyojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 600,Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe wa Wilaya ya Hai,Dk Itikija Msuya alisema ujenzi wake ulianza mwaka 2010 na utakamilika Septemba mwaka huu na kitahudumia zaidi ya wananchi 14,000.
Dk Msuya alisema wananchi walianza kujenga kwa kuchangisha fedha shilingi milioni 11 kisha halmashauri ikaongeza Sh milioni 28 na ndipo serikali kuu kupitia fedha za tozo ya miamala ikapeleka Sh milioni 500,000 katika awamu mbili.
Amesema hadi sasa jengo la wagonjwa wa nje,maabara na kliniki ya baba,mama na mtoto na nyumba za watumishi tatu umekamilika huku awamu ya pili ya ujenzi kwa ajili ya kuongeza majengo ya upasuaji,wodi ya wazazi na jengo la kufulia mafundi wameshapatikana na ujenzi utakamilika Septemba mwaka huu.
Akizungumzia manufaa ya kituo hicho cha afya,Zubena Hussein mwananchi wa Chekimaji aliishukuru serikali kuwaletea huduma ya afya karibu kwa sababu walilazikima kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo Bomang’ombe
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇