Na Mwandishi Maalum, Zanzibar
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa Mjini (Kichama), Talib Ali Talib, ameitaka jamii kujenga tabia ya kutembelea wagonjwa wakati wa matukio maalum ya kitaifa ili kuimarisha imani na mapenzi miongoni mwao.
Talib alieleza hayo alipotembelea wodi za wazazi za hospitali ya Mnazi Mmoja na Mwembeladu, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na kukabidhi zawadi mbali mbali kuwapongeza wazazi hao na kuhamasisha zoezi la sensa ya watu na makaazi lililoanza jana.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Talib alisema alisema pamoja na kuhamasisha ushiriki wa makundi yote kwenye sensa, ametoa zawadi hizo kushereheka siku yake ya kuzaliwa pamoja na watoto hao.
Alisema watoto waliozaliwa katika siku hiyo watakuwa na historia kubwa nchini na kwamba watalikumbuka zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi na ustawi wa watu wake.
“Hawa ni miongoni mwa watanzania walioingia kwenye hisabu kupitia sensa hii hivyo bila shaka watakuwa na kumbukumbu isiyosahaulika kama ilivyo kwa watu wote waliojitokeza kushiriki zoezi hili,” alieleza Talib.
Aidha alitoa wito kwa wananchi ambao hawajafikiwa na makarani wa sensa kuendelea kuwa wavumilivu na kufuata maelekezo yaliyotolewa na ofisi za takwimu ya kuacha taarifa zao majumbani mwao kurahisoisha upatikanajai wa taarifa zao.
Nae Daktari Mkaguzi wa hospitali ya Mnazimmoja, Nadya Nassor Gharib, alimpongeza mwenyekiti huyo na viongozi wengine wa chama alioambatana nao kwa kuona umuhimu wa siku hiyo, na kukumbuka watoto waliozaliwa.
Alisema hadi kufikia majira ya saa 8 mchana, watoto 47 walikua wamezaliwa hospitalini hapo ambapo 36 walipatiwa za nguo na vyandarua vya watoto.
“Wazazi waliopokea zawadi hi bila shaka wamefarajika na kufurahia uwepo wao lakini tunamshukuru Mwenyekiti kwa kuamini kuwa kupitia yeye watu wengine watajitokeza na kusaidia upatikanaji wa baadhi ya huduma,” alisema Nadya.
Kwa upande wake Muuguzi na Mkunga katika hospitali ya Mwembeladu, Khadija Ramadhan Kassim, alisema katika usiku huo walipokea wazazi sita waliojifungua watoto sita wakiwemo wannne wa kike.
Alisema ujio wa Mwenyekiti Talib, umetoa faraja kwa madaktari na wazazi waliofika hapo, aliwataka viongozi wengine kujitokeza kusaidia baadhi ya vifaa ili kuboresha huduma za wananchi.
Akizungumza baada ya kupokea zawadi hizo, mmoja ya kimna mama hao, Munta Nassor Mohammed mkaazi wa Mwanakwerekwe, aliwapongeza madaktari na wauguzi wa hospitali ya mnazimmoja kwa huduma walizompatia.
“Huyu ni mtoto wangu wa sita, nashkuru jinsi madaktari walivyonihudumia toka nilipofika na zawadi alizotupa kiongozi zimeongeza furaha yangu na pengine kila mmoja hapa,” alieleza mama huyo aliyejifungua mtoto wa kiume.
Watoto 53 walizaliwa kwenye siku ya kwanza ya zoezi la sensa ya watu na makaazi katika hospitali hizo ambapo walipatiwa zawadi za nguo na vyandarua kwa ajili ya watoto waliozaliwa katika hospitali za Mnazimmoja na Mwembeladu, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇