LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 25, 2022

WAZIRI NDALICHAKO ATOA TAMKO KUHUSU TISHIO LA MGOMO WA MADEREVA

 


Ndugu Wanahabari; Kama mnavyokumbuka mnamo tarehe 22 Julai, 2022 Serikali  ilitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia Hoja na Malalamiko yaliyowasilishwa na Viongozi wa Vyama vya  Wafanyakazi Madereva na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji nchini. 

Kufuatia  kutolewa kwa taarifa hiyo, wapo baadhi ya Madereva ambao wameipokea kwa  mtazamo tofauti. Kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakipotosha taarifa hiyo na  kuchochea ama kuhamasisha Madereva wenzao kugoma. Uchochezi wa mgomo wao  umejikita katika viwango vya posho ambavyo Madereva, Wamiliki wa Vyombo vya  Usafiri na Serikeli waliafikiana katika vikao vya majadiliano. 

Ndugu Wanahabari; Viwango walivyokubaliana ni viwango vya chini vya posho za  safari (Minimum allowances) ambapo waajiri hawaruhusiwi kulipa chini ya viwango  hivyo. Kwa wale Waajiri ambao walikuwa wanalipa viwango ambavyo viko juu ya  viwango vya chini vya posho za safari vilivyowekwa, hawaruhusiwi kushusha viwango  hivyo kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa Sheria.

Ndugu Wanahabari; Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya usafirishaji kwa uchumi  wa nchi, inasisitiza kuwa nafasi ya majadiliano bado ipo wazi na hivyo Wafanyakazi  Madereva ambao wana hoja na malalamiko zaidi ya yale yaliyofanyiwa kazi, wayawasilishe rasmi katika mamlaka zinazohusika ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.  

Ndugu Wanahabari; Ninawasihi Wafanyakazi Madereva wapokee kwa mtazamo chanya  taarifa ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia Hoja na Malalamiko  yaliyowasilishwa na Vyama vyao na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji. Ninawasihi Wafanyakazi Madereva wote kuendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida. Natoa rai  kwa makundi yanayojihusisha kuchochea migomo ya Madereva kuacha mara moja, kwani  kufanya hivyo ni kukiuka Sheria. Hivyo, Serikali haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wale  wote watakaoendelea kuchochea migomo ya Madereva. 

IMETOLEWA NA  

Prof. Joyce Lazaro Ndalichako (MB) 

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU 

(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU) 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages