************************
Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inakwenda kuandika historia baada ya kutenga fedha zaidi ya Sh.bilioni 600 kwa ajili ya kujenga upya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Shaka ametoa kauli hiyo leo Julai 2,2022 alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) ambapo pamoja na mambo mengine ameipongeza Serikali kwa namna ilivyoboresha mazingira ya utoaji huduma za afya katika taasisi hizo.
Akifafanua zaidi Shaka amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeshatenga fedha hizo kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo unaokwenda kujenga historia katika sekta ya afya nchini huku akielezea kufurahishwa kwake na mikakati iliyowekwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kufanikisha ujenzi huo.
“Uwekezaji huu ambao umewekwa katika sekta ya afya sasa umenza kuzaa matunda na kwenye hili nichukue fursa hii kwa dhati kabisa kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya” amesema Shaka
Amefafanua Hospital ya Muhimbili iliyoanzishwa Mwaka 1905 wakati ikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa karibia 10100 kwa mwaka na sasa hivi inahudumia watu zaidi ya 3000 kwa siku lakini kutokana na kazi kubwa iliyofanywa kwa Awamu tofauti kuanzia awamu ya kwanza hadi sasa Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kumeonyesha dhamira ya dhati ya kuwekeza katika sekta ya afya
Ameongeza akiwa kwenye ziara hiyo ametembelea taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na vitengo vyake pamoja na Hospitali ya Muhimbili na vitengo vyake na kujionea namna ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyowekeza katika vifaa tiba pamoja na watoa huduma wakiwemo wataalam mbalimbali.
“Tumeona madaktari bingwa kabisa waliosomeshwa na Serikali lakini tumeona uwekezaji uliofanywa katika vifaa tiba na kupitia fedha za ahueni ya uviko 19 zimefanya mageuzi na Mapinduzi makubwa Muhimbili ikiwemo ununuzi wa mashine za kisasa ” alisema Shaka
Amesema kwa kiujumla uwekezaji mkubwa katika taasisi hizo mbili umewezesha kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafiri kwenda kupatba matibabu nje ya nchi kwa wastani wa asilimia 97 suala alilosema pongezi zinapaswa kwenda kwake Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoisimamia na kuitekeleza ipasavyo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Amesema mbali na Taasisi hizo kutoa matibabu kwa watanzania pia imekuwa ikiwahudumia raia kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo ya Rwanda, Burundi,Congo na nchi zingine za Afrika hatua iliyoziwezesha nchi za Afrika kupunguza gharama za kuwasafirisha wagonjwa nje ya Bara la Afrika kwa wastani wa Dola Milioni 1.6.
Katika hatua nyingine Shaka alitumia nafasi hiyo kuzungumza na Mzazi wa Watoto mapacha waliotengenishwa Amina Amosi(18) Mkazi wa Simiyu aliyepo Hospitalini hapo ambapo alimtia moyo huku akitoa maelekezo kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii kutembelea mzazi huyo na kumueleza namna ambavyo Serikali itamsaidia malezi ya Watoto.
Awali Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Aminiel Elgaesha amesema Hospitali ya Muhimbili imefanya upasuaji huo kwa mafanikio makubwa huku hali zao zikiendelea vizuri chini ya uangalizi wa jopo la madaktari
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇