LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 9, 2022

KATIBU MKUU PROF. KATUNDU AWAKUMBUSHA WAAJIRI KUJISAJILI NA KUWASILISHA MICHANGO WCF

Na Mandishi Maalum, Sabasaba
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu amewakumbusha waajiri kote nchini kujisaliji kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kuwasilisha michango kwa wakati.

 

Amessisitiza kwamba hilo ni muhimu kwa kuwa kufanya hivyo watakuwa wametekeleza haki ya msingi ya mfanyakazi kufidiwa pindi anapoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

Profesa Katundu ametoa wito huo Julai 8, 2022 baada ya kutembelea banda la WCF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba jijini Dar es Salaam.

“Ni haki ya msingi ya mfanyakazi, kwa mwajiri wake kujisajili kwenye Mfuko wa WCF na kuhakikisha kwamba michango anawasilisha kwa wakati ili malengo yaliyokusudiwa ya kuanzishwa kwa Mfuko yaweze kutekelezeka.” Alifafanua Profesa Katundu.

Alisema amefurahishwa na jinsi watumishi wa WCF wanavyotoa huduma kwa wananchi kwani kila dawati alilopita ameona jinsi wananchi wanavyohudumiwa kwa kupatiwa elimu na ufafanuzi mbalimbali kuhusu masuala ya fidia na shughuli za Mfuko kwa ujumla wake.

Miongoni mwa huduma zitolewazo kwenye banda la WCF lililoko mtaa wa Mabalozi, ni pamoja na elimu kuhusu jinsi ya kujisajili na Mfuko kwa kutumia Mifumo ya kisasa ya TEHAMA, kuwasilisha michango, jinsi ya kutoa taarifa pindi mfanyakazi anapoumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi, lakini pia jinsi tathmini ya ulemavu inavyofanyika, alisema Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Elimu kwa Umma, WCF Bi. Laura Kunenge.

“Tumejipanga kuhakikisha tunawahudumia wateja wetu ( waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla) kuhusu uelewa wa jumla wa Mfuko na huduma zetu tunazotoa hapa ni kama zile zinazopatikana kwenye ofisi zetu za Makao Makuu na Kanda.” Alifafanua.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya Maonesho hayo yaliyoanza Juni 28 na yanayotarajiwa kufikia kilelel Julai 13, 2022, ni “Tanzania Mahali Sahihi Pa Biashara ya Uwekezaji.”.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu (kulia) akipokea majarida na nembo ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kutoka kwa Meneja Mipango WCF,  Patrick Ngwila alipotembelea kwenye banda la Mfuko huo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, jana Julai 8, 2022.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu (kulia) akitembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, jana Julai 8, 2022.

Profesa Katundu akisaini kitabu cha Wageni huku akiwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Mhe. Abdallah Mtinika (wapili kushoto) na kushuhudiwa na Mwanasheria Mwandamizi WCF, Bw. Deogratius Ngowi.

Mstahiki Meya wa Temeke, Mhe. Abdallah Mtinika (kulia) akiagana na Meneja Mipango WCF, Bw. Patrick Ngwila na Bw. Imani wakati akiondoka kwenye banda la Mfuko baada ya kulitembelea

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages