Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusu eneo la Hifadhi ya Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, bungeni jijini Dodoma, Juni 10, 2022.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Asisitiza hakuna kijiji kitakachohamishwa tarafa ya Loliondo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania na wana-Loliondo kupuuza upotoshaji unaofanywa na baadhi watu wasiolitakia mema Taifa kuhusu eneo la hifadhi ya Loliondo lililopo Tarafa ya Loliondo na badala yake waendelee kuisikiliza Serikali.
“Kilichotokea si uhalisia, hakuna tishio lolote, wale wameenda msituni kuweka alama katika eneo ambalo liko mbali sana kijiji cha karibu kipo umbali wa kilomita nane, wananchi waendelee na shughuli zao, wasisikilize upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya nchi hii, hakuna mapambano yoyote, hakuna askari yeyote aliyekwenda huko kijijini kutishia amani.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Juni 10, 2022 wakati akitoa kauli ya Serikali Bungeni jijini Dodoma kuhusu taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusu eneo la hifadhi ya Loliondo wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Amesisitiza kwamba wananchi watulie na Serikali haina lengo la kumhamisha mtu, vijiji vyote 14 vitaendelea kuwepo.
Amesema kuwa Serikali inaamini wale wanaofanya hamasa za vurugu katika eneo la Loliondo wataacha mara moja kufanya hivyo ili kuwaacha wananchi waendelee na shughuli zao. “Wanapaswa kufahamu kwamba wanapeleka usumbufu mkubwa kwa kina mama, wazee na watoto, Serikali ipo macho dhidi yao.
“Nataka niwaambie Serikali ipo macho na hatuta muonea mtu yeyote. Wananchi watulie hakuna shughuli yoyote ya kumuhamisha mtu, hatuna lengo la kumuhamisha mtu kwenye eneo la Loliondo. Lile eneo ni letu sote na tutaliratibu vizuri. Alama zinazowekwa ni wigo wa kuonesha mpaka ambayo kwa pamoja tutaitumia kulinda na kulihifadha eneo lile.” Alisema eneo hilo lipo umbali wa kilomita nane kutoka kijijini.
Amesema shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali katika eneo lenye vijiji ni pamoja na uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa majosho na mabakuli ya kunyweshea mifugo. Amesema Watendaji wa Wizara ya Maji na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wapo katika maeneo hayo wakiendelea na kazi.
Wakati huohuo, Akizungumzia kuhusu Tarafa ya Ngorongoro, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari kaya 293 zenye watu 1,497 zimeshajiandikisha kwa ajili ya kuhama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia katika kijiji cha Msomera kilichoko wilaya ya Handeni mkoani Tanga ili kupisha uhifadhi endelevu wa Hifadhi ya Ngorongoro
Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Akson ameishauri Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika na upotoshaji huo. “Pamoja na elimu kutolewa mara kwa mara, uposhaji bado unaendelea kwa sababu hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wanaofanya upotoshaji huo hasa wale walioko hapa nchini.”
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇