LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 28, 2022

AG DK. FELESH AWAFUNDA VIONGOZI WAPYA TLS, AWAASA KUWA NA MIFUMO YA KIUTENDAJI ITAKAYORAHISISHA USHIRIKIANO NA OFISI YAKE

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi, amewafunda Viongozi wapya wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania Bara (TLS) ikiwemo kuwapa rai ya kuwa na mifumo bora zaidi ya kiutendaji ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia na kurahisisha ushirikiano kati ya Chama hicho na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

AG Jaji Dk. Feleshi ametoa amewafunda na kutoa rai hiyo hivi karibuni, wakati akizungumza na Ujumbe wa Baraza la Uongozi wa TLS ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Prof. Edward Hosea, ulipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma
, kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo  kufuatia uchaguzi wa viongozi wa Chama hicho uliofanyika hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, Uongozi  wa TLS uliwasilisha hoja mbalimbali ambazo walimuomba AG Jaji Dk. Feleshi kuwasaidia kuzifutailia, zikiwa ni pamoja na ombi la kurejeshwa sehemu ya malipo ya wanachama wao zinazolipwa Mahakamani, ombi ambalo walisema kwa msaada wake linaendelea  vizuri.

“Nawapongeza kwa kuchaguliwa,  wanachama wenu wamewaamini, TLS ni  mdau muhimu katika  tasnia ya  sheria na hususani katika utawala wa sheria, hivyo nawaomba muwe na mifumo mizuri ya kuitendaji ambayo pamoja na mambo mengine itawezesha kubaini mawakili wabobezi katika maeneo mbalimbali ambao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapenda kuwatumia pale itakapohitaji kufanya hivyo” akasisitiza  AG Dk. Feleshi.

Kuhusu  hoja  ambazo TLS wameomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusaidia kuzifutalia, AG Feleshi   ameahidi  kuendelea kuwasaidia kufuatilia  kwa baadhi ya hoja ambazo zimo ndani ya mamlaka yake, ikiwamo ya kiwanja, ahadi ambayo aliitoa mbele ya Rais Samia  Suluhu  Hassan.

Aidha kwa  hoja ambazo zipo nje ya mamlaka yake zikiwamo  za  mabadiliko ya kisheria ili pamoja na mambo mengine, kuongeza muda wa kufanya uchaguzi wa viongozi wa TLS, ameutaka uongozi huo kufuatilia katika     Taasisi husika  ikiwamo Wizara ya Katiba na Sheria.

AG Dk. Feleshi ameahidi utayari wa Ofisi yake wa kushirikiana na  TLS katika  kutekeleza majukumu ya kisheria kwa maslahi mapana ya umma wa Watanzania na akawataka TLS kuwa mabalozi na jicho katika utekelezaji wa majukumu hayo.
 
 Kwa upande wao  Uongozi TLS, pamoja na mambo mengine ulitumia nafasi hiyo kumpongeza kwa mara nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuteuliwa kwake kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na  kumshukuru kwa namna ambavyo amekuwa tayari  kushirikiana na TLS ikiwa ni pamoja na kusukuma mbele hoja zao mbalimbali.

AMwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi akizungumza na Ujumbe wa Baraza la Uongozi wa wapya wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania Bara (TLS) ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Prof. Edward Hosea, ulipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma, kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo, hivi karibuni. (Picha na Mpigapicha Maalum)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages