LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 11, 2022

WATOTO UMRI CHINI YA MIAKA MITANO KUPATIWA CHANJO YA UGONJWA POLIO NCHI NZIMA, KUANZA MEI 18 HADI 21…WIZARA YATOA NENO

 Na Mwandishi Wetu.


WATOTO wenye umri chini ya miaka mitano nchi nzima wanatarajia kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa kupooza maarufu kwa jina la Polio kuanzia Mei 18 hadi 21 mwaka huu.

Hayo yameelezwa leo Mei 11 jijini Dar es Salaam wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa Wahariri, waandaji wa vipindi pamoja na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali .

Semina hiyo ilikuwa na lengo la kuelezea kampeni ya kuanza kwa chanjo hiyo ili kuhakikisha vyombo vya habari vinafikisha taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo ya polio.

Akizungumza kwenye semina hiyo ,Kaimu Mkuu wa kitengo Cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya afya Catherine Sungura amesisitiza kampeni ya chanjo itazinduliwa rasmi tarehe 18 na itafanyika kwa siku nne, hivyo itamalizika terehe 21 ya mwezi huu na lengo nikuwafikia watoto wote chini ya miaka mitano nchi nzima.

“Kwa hiyo tumewaita hapa kwa kutambua ninyi ni wadau muhimu kwani tunao Wahariri, Waandaaji wa vipindi na waaandishi wa habari kwa hiyo tunajua kupitia vyombo vya habari wananchi watafahamu umuhimu wa chanjo hiyo.

“Hivyo kupitia semina hii tutakaa na kuelewa ili kufikisha ujumbe sahihi na vema ikafahamika chanjo hii ni ya kawaida na huwa inatolewa mara kwa mara kwani hata wajawazito wanapojifungua watoto lazima wapate chanjo hii,”amesema.

Ameongeza mtoto anapozaliwa hadi anapofikisha miaka mitano wamekuwa wakipatiwa chanjo hiyo, hivyo ni ya kawaida na iko salama.”Baada ya Wizara kutangaza chanjo hii kuwa itafanyika nchi nzima kuna baadhi ya watu wamekuwa na mashaka na wanaona kama haiku salama, ukweli chanjo hii ni salama na haina tatizo lolote, kazi ya Wizara ni pamoja na kulinda afya za Watanzania.”

Ameongeza wazazi au walezi wanatakiwa kufahamu chanjo hiyo ni ya kawaida na vema wakahakikisha watoto walio na umri chini ya miaka mitano wanaipata.

Akielezea zaidi chanjo hiyo ya ugonjwa wa kupooza amesema mwanzoni waliitoa katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe, waliitoa huko kwasababu kulikuwa na kuna mlipuko katika nchi ya Malawi na Tanzania sio kisiwa.“Tunafahamu mikoa hiyo iko pembezoni hivyo tukasema kwamba kuna muingiliano wa nchi hizi mbili.Kampeni ya awali katika ile mikoa ilifanikiwa lakini sasa tumeona tutoe chanjo hii kwa watoto chini ya miaka mitano katika nchi nzima.”amesema.

Kwa upande wake Afisa Mradi wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bi. Lotalis Gadau alibainisha kuwa, lengo la zoezi hilo  ni kutoa chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 wapatao Milioni 10,567,805.

"Tayari chanjo zaidi ya Milioni 13, tumezipata na tutaendesha zeozi kwa siku Nne, Mei 18 hadi 21 mikoa yote kwa watoto wa chini ya miaka 5.

Zoezi litakuwa la awamu Tatu, kwa mwezi Mei, June,  na Julai, lakini kutakuwa na wasimamizi wa Kitaifa katika mikoa yote kusaidia mikoa kuendesha kampeni,na kampeni hiyo itaendeshwa nyumba kwa nyumba." alisema Gadau.

Aidha, Mpango wa Taifa wa Chanjo ulianzishwa mwaka 1975 huku ukiwa na Chanjo 12 zinazozuia Magonjwa wanazotoa hapa nchini.

Kuhusu Polio, ambao ni ugonjwa wa unaosababishwa na virusi vya Polio ambapo kwa kawaida unasababisha kupooza na baadae kifo, ambapo pia ugonjwa huu uathiri watu wa rika zote lakini watoto wadogo uathirika zaidi.

..ugonjwa huu hauna tiba, lakini unaweza tu kuzuiliwa tu kwa kupata chanjo ya matone ya Polio au ya sindano." alisema Gadau.

Ugonjwa huo wa Polio umekuwa na viashiria mbalimbali ikiwemo: Ulemavu wa ghafla, tepetepe kwa viungo kama mikono ama miguu, kulegea kwa kiungo kukosa nguvu, kushindwa kunyanyua miguu ama mikono.

Mtoto kushindwa kukaa, kushindwa kutembea/kuchechemea, kuvuta mguu na mengine mengi.

Aidha, kampeni hizo zinakuja kufuatia kuibuka kupatikana kwa mgonjwa, Lilongwe, Nchini Malawi mnamo Februari 17, mwaka huu hivyo, Wizara ya Afya Nchini ikaonelea kuchukua juhudi za haraka ilikulinda wananchi wake zaidi dhidi ya ugonjwa huo wa Polio hasa kwa watoto wadogo.


Kaimu Mkuu wa kitengo Cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya afya Catherine Sungura akizungumza leo Mei 11 jijini Dar es Salaam wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa Wahariri, waandaji wa vipindi pamoja na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali kuhusu utoaji chanjo ya Polio kwa njia ya Matone Watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchi nzima kuanzia Mei 18 hadi 21 mwaka huu.

Afisa Mradi wa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bi. Lotalis Gadau akifafanua jambo  wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa Wahariri, waandaji wa vipindi pamoja na wanahabari (hawapo pichani) kutoka vyombo mbalimbali leo Mei 11,2022 jijini Dar es Salaam,kuhusu lengo la kutoa chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 wapatao Milioni 10,567,805.

Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Dar es Salaam,Juma Haule akizungumza leo Mei 11 jijini Dar es Salaam wakati wa semina maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa Wahariri, waandaji wa vipindi pamoja na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali kuhusu utoaji chanjo ya Polio kwa njia ya Matone Watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchi nzima kuanzia Mei 18 hadi 21 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages