Na CCM Blog, Arusha
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwito kwa waandishi wa habari kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya uchapishaji wa picha za utupu mitandaoni kwa kuwa baadhi hufanya hivyo kwa kukosa elimu, huku akiwataka pia kujilinda wenyewe badala ya kusubiri walindwe na sheria.
Rais Samia ametoa mwito huo leo Jumanne Mei 3, 2022 wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari katika ukumbi wa Gran Melia Hotel Jijini Arusha.
“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri (Nape Nnauye) sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote”, amesema Rais Samia.
"Waziri (Nape) amesema pale kwamba tunatumia busara lakini sheria zipo pale pale, busara ninayotumia, ukinikuna vizuri mimi nitakukuna na kukupapasa huku nakupuliza ufuuuu lakini ukipara nitakuparura, twende tufanye kazi kwa uungwana, twende tufanye kazi kwa kuelewana", amesema Rais Samia.
Waandishi wa habari mna mchango mkubwa katika maendeleo, kwanini mimi nifanye kazi bila waandishi wa habari. Hivyo hatuhitaji kugombana, tukae tuzungumze tujenge nchi yetu",amesema Rais Samia.
Akizungumzia kaulimbiu ya Siku hiyo ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ambayo ni ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti', Rais Samia alisema, miongoni mwa changamoto ni matumizi mabaya ya mitandao ikiwemo baadhi ya watu kujiweka humo picha ambazo zinakiuka maadili hasa ya Kitanzania.
Amesema wanaoweka picha hizo mitandaoni sio tu wanajidhalilisha wenyewe, bali pia wanadhalilisha familia zao na Tanzania kwa ujumla, hivyo hawana budi kuacha mtindo huo kwa kuwa wanachoweka mitandaoni kinaonekana hata kwa watoto, na hivyo wana momonyoa maadili.
"Hebu jaribu kujifiria, kama unakuta picha ya dada yako mtandaoni amejianika, hivi utajisikiaje?", alisema na kuhoji Rais Samia.
Alisema, Waabdishi wa habari Barani Afrika inawapasa kuzingatia uzalendo wanapoandika habari zao akiwashangaa kwa nini hawaandiki mambo mema yaliyomo katika Bara la Afrika ikiwemo utalii na maliasili nyingi kila eneo.
"Bara la Afrika limekuwa ni bara la kuandikwa maovu tu, linaimbwa na kuandikwa habari za umasikini, hadi inaonekana kama Afrika ndiko kwenye umaikini wa akili, wa mali, lakini ukiangalia kwa ndani si kweli.
Nilikuwa nabishana na wakuu wa uchumi huko, nikawaambia kwamba nchi yangu haiishi kwa Dola moja kwa siku, wakaniambia kivipi? Nikawapa mfano wa makabila ambayo sisi tunasema yako chini kama ya wale wanaokula matunda tu na nguo zao ngozi na ili aishi anakula matunda siku nzima na asali lakini hivi vitu ni "organic" ambavyo ukienda "supermarket ya Ulaya ni ghali, utasemaje wananchi wangu wanaishi kwa Dola moja kwa siku?", akasema Rais Samia.
"Leo hii kuna katuni zilizoko mitandaoni hazina maadili katika nchi yetu, na tunajua vile watoto wanavyopenda katuni, Unakuta mwanaume kwa mwanaume wanabusiana, mwanamke kwa mwanamke wanashikana lakini ni katuni ambazo hatuzisimamii.
Tunaacha watoto wanaangalia, mtoto anazaliwa leo ukimwekea iPad anafungua na wanatizama kila kitu, kafundishwa na nani hujui, Lakini Waziri wizara yako haichuji tunajenga watoto wa taifa lipi, Mila zetu zinaruhusu watoto waone hayo? kila kitu ni mpaka Rais aseme?. Nendeni kafanyeni kazi yenu", akasema Rais Samia.
Rais Samia akizungumza na Wadau wa vyombo vya habari na Waandishi wa habari jijini Arusha, leo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇