Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Rufiji. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetekeleza ahadi zote ilizotoa kwa wananchi wa Rufiji na amewataka waendelee kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya maendeleo ya kitaifa ikiwa ni pamoja na zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, 2022 ilikuboresha maisha yao kwa ujumla.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo Mei 2, 2022 baada ya kukamilisha zoezi la mbio za Mwenge katika Wilaya ya Rufiji ambalo lilianza jana na kukagua miradi mbalimbali katika Wilaya hiyo.
Akimkaribisha Kiongozi wa mbio za Mwenge kwenye jimbo lake la Rufiji jana, Mhe. Mchengerwa amesema tayari miradi yote iliyopangwa katika eneo hilo kulingana na bajeti imetekelezwa ambapo hadi sasa utekelezaji wa miradi ya maendeleo umefikia asilimia 136.
"Ndugu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2022, kwanza kabisa naomba nikukaribishe katika eneo letu la Rufiji, lakini pili nipende kumshukuru Rais wetu kwa kukamisha ahadi zote ilizotoa wakati wa uchaguzi". Amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Pia ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilometa 37 ya Nyamwage- Utete kwa kiwango cha lami na Ikwiriri- Mkongo yenye kilometa 31.
Aidha ameongeza kuwa hadi sasa Halmashauri ya Rufiji imebakiwa na akiba ya zaidi ya 1.5 bilioni.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa kuendelea kuwaletea makubwa wananchi wa Rufiji.
Akizungumza kwenye mradi wa uzinduzi wa ghala la kuhifadhia zaidi ya tani 300 katika eneo la mkombozi amesifu jitihada za Mhe. Mchengerwa za kushirikisha sekta binafsi kuwekeza katika miradi ambayo inawasaidia wananchi.
Geraruma amezitaja salamu za mbio wa Mwenge wa mwaka huu kuwa ni pamoja na wananchi kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa linasaidia pamoja na mambo mengine uundaji wa Sera na Mipango ya Serikali.
Salamu nyingine ni kupima virusi vya UKIMWI, kujikinga na malaria, kuepuka madawa ya kulevya na rushwa pamoja na kuzingatia lishe bora ili kuepukana na udumavu.
Mhe. Mchengerwa pia ameshiriki kwenye risala ya utii kwa Mhe. Rais wakati wa mbio hizo za Mwenge wa Uhuru.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇