LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 22, 2022

LUSINDE: ZITTO NA WENGINE WANAOMNANGA HAYATI DK. MAGUFULI NA KUMSIFU RAIS SAMIA NI WACHONGANISHI NA WANAFIKI WAKUBWA

Bungeni, Dodoma
Mbunge wa Mvumi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Livingstone Lusinde, amecharuka na kusema Kiongozi wa ACT- Wazalendo Zitto Kabwe na wengine wanaomsema vibaya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli na kumsema vizuri Rais Samia Suluhu Hassan ni wachonganishi na wanafiki wakubwa.

Lusinde amesema, Zitto na hao wengine wanaomsema vibaya hayati Magufuli na kumsifu Rais Samia ni wachonganishi na wanafiki wakubwa kwa sababu hata Rais Samia naye watakuja kumsema vibaya  pindi atakapoondoka madarakani kwa kuwa ndiyo tabia yao.

Lusinde ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 22, 2022 Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi ya Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2022/2023.

Amesema licha ya ushirikiano uliopo kati ya vyama vya CCM na ACT Wazalendo Visiwani Zanzibar, ameshangazwa na Zitto kumnanga Hayati Dk. Magufuli kana kwamba Zitto hashiriki katika Serikali ya Zanzibar.

“Nataka niseme,  Marehemu Magufuli aheshimiwe, kufiwa ni suala kubwa haiwezekani kulizungumza kwenye utawala bora suala la Magufuli kusemwa vibaya na mimi sitaacha.

Zitto anatutaka tunaompenda Magufuli tukazikwe naye, yeyeo amewahi kufiwa na mama yake mimi sitaki kuingia huko mama wa Zitto ni mama yangu mimi ametanguliwa, Mimi nimewahi kufiwa na Baba yangu lakini ACT Wazalendo wamewahi kufiwa na Maalim Seif wanataka tumseme vibaya sisi hatuwezi,”akasema Lusinde.

Amesema Wabunge walio wengi ni Waislamu wamefungwa na dini inakaata kuwasema vibaya marehemu na Zitto anajua hilo.

Amesema Zitto amewakosea sana Watanzania, Mke na familia ya Magufuli anatakiwa kuwaomba radhi kwa kitendo chake cha kumnanga Magufuli.

Lusinde, amesema wasifikiri kumsema vibaya Magufuli kutawasaidia kwa sababu ameshafariki dunia na kwamba kama mtu alikuwa na tatizo naye amalize watakuja kukutana naye kwa Mungu.

“Mtu akishatangulia kitabu chake kinafungwa tunamuachia Mwenyezi Mungu kuja kutoa hukumu, inakuaje viongozi wakiwepo hamsemi wakiondoka mnasema huo ni uoga uliopitiliza,” Akasema Lusinde.

Lusinde amesema mtu mmoja alisema kwa vitendo kuwa hawezi kufanya kazi na Magufuli naye alikuwa ni Nyalandu (Lazaro Nyalandu aliyewahi kuwa Mbunge wa Singida Kaskazini na Waziri wa Maliasili na Utalii).

“Lakini wote tuliobaki hapa ni watu wa Magufuli, na tulifanya naye kazi na tulikuwa tunamsifu na hivyo ndivyo tunatakiwa kumsifu na mheshimiwa Samia (Rais Samia Suluhu Hassan). Ndio kazi tunayoifanya hapa hatufanyi unafiki.

Nataka nikwambie, hawa watu wanaomsema vibaya Magufuli na kumsifu Rais Samia ni wanafiki wakubwa, Samia akiondoka watamsema vibaya hivyo hivyo, ni bora mimi Lusinde niko wazi na siwezi kuacha haiwezekani.” akasema.

Lusinde ambaye pia ni maarufu kwa jina la Kibajaji, amesema ili nchi iendeleze utawala bora ni lazima watu wote kushirikiana nao na kwamba hao waliofariki dunia ni watu wazito.

Amehoji kauli ya wanaompenda Magufuli wakazikwe naye maana yake ni nini, na kumtaka Zitto kuomba radhi na asirudie tena kusema maneno hayo ya kipuuzi. Hivi karibuni Zitto amekaririwa kwenye mitandao kadhaa ya kijamii akiwakosoa wanaomsifia Hayati Rais Magufuli akisema "Wanaompenda wakazikwe naye!".


Livingstone Lusinde

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages