************************
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Geraruma,ametembelea mradi wa maji safi na salama katika kijiji cha Nangomba uliojengwa na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijiji(Ruwasa)wilaya ya Nanyumbu.
Geraruma,amewapongeza Wahandisi na watendaji mbalimbali wa Ruwasa wilayani humo, kwa kutekeleza vyema ujenzi wa mradi huo wa maji ambao umetimiza lengo la Serikali la kumtua mama ndoo kichwani.
Geraruma ametoa pongezi hizo jana,mara baada ya kutembelea mradi huo umetekelezwa kwa lengo la kumaliza changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji viwili vya Nangomba na Mjimwema.
“Wahandisi wa Ruwasa nawapongeza sana kwa kuendelea kujenga na kusimamia mradi huu,mmefanya kazi nzuri sana,Serikali kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 inawapongeza”alisema.
Alisema, wataalam hao wameonyesa namna watendaji wa taasisi za umma wanavyotakiwa kutimiza wajibu wao katika kujenga na kusimamia miradi muhimu ya maendeleo katika jamii.
Amewataka kuendelea kuchapa kazi,kutanguliza uzalendo,kuwa makini na kuhakikisha miradi yote inayojengwa ina kuwa na ubora na viwango vinavyotakiwa.
Amewataka wataalam wa taasisi nyingine za umma katika mkoa wa Mtwara,kujifunza kwa Ruwasa namna miradi inavyojengwa pindi wanapopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo yenye lengo la kuwaondolea wananchi kero na kuharakisha maendeleo ya nchi.
Aidha,ameishukuru familia ya mkazi wa kijiji cha Nangomba Said Abdul kwa uzalendo wake kufuatia kutoa eneo lililojengwa mradi huo bure, na kumuagiza meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha kupeleka huduma ya maji kwa familia hiyo bila gharama yoyote.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilayani Nanyumbu Simon Mchucha alisema,mradi huo umetekelezwa katika vijiji vya Nangomba na Mjimwema kata ya Nangomba kupitia program ya malipo kwa matokeo(PforR) kwa gharama ya Sh.196,430,118.06.
Alisema, chanzo cha mradi ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 6,000 kwa saa na unahudumia zaidi ya wananchi 5,151 katika vijiji vya Nagomba na Mjimwema.
Mchucha alieleza kuwa,ujenzi wa mradi huo umehusisha vituo 11 vya kuchotea maji,ukarabati wa tenki la lita 50,000 nyumba ya mitambo, nyumba ya mlinzi,ununuzi wa pampu na Jenereta na kaya 23 zimeunganishiwa huduma ya maji.
Alitaja mafanikio mengine ni ukusanyaji mapato yanayotokana na mauzo ya maji ambapo wastani kwa mwezi ni Sh.1,270,530 ambapo fedha zilizokusanywa tangu mradi ulipoanza kutoa huduma Mwezi Oktoba 2021 hadi Machi 2022 kufikia Sh.8,892,285.
Mhandisi Mchucha alisema,mradi huo unaendeshwa na wananchi kupitia Jumuiya ya watumia maji(NAMJI)ambapo chombo cha watoa huduma za maji ngazi ya jamii kimefanikiwa kutoa ajira kwa watu 15 kati yao wanaume 2 na wawanawake 13.
Kwa mujibu wake,Ruwasa kupitia vikao na mikutano yam aji inayofanyika sehemu mbalimbali inawahamasidha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye zoezi maalum la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Mwezi Agosti Mwaka huu.
Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahaya Mhata alisema,huo ni mradi mkubwa kutekelezwa na Ruwasa katika Jimbo la Nanyumbu na ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ambazo zimefanikilisha kujengwa kwa mradi huo.
Amewaasa wanufaika na wananchi kwa jumla,kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya vizazi vya sasa na vinavyokuja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇