Na Dismas Lyassa, Kibaha
HUENDA shida kubwa ya maji ambayo imekuwa ikiwasumbua wananchi wa mitaa iliyoko Kata Pangani, Halmashauri ya Mji Kibaha, Mkoani Pwani ikabaki historia kufuatia mradi wa maji Vikawe kukamilika kwa asilimia 88.
Diwani Mdachi pichani akifafanua jambo
Wengi wa wananchi wa mitaa hiyo wanatumia maji ya mto Mpiji ambayo sio salama kwa matumizi kwa wanadamu. Wengine hutumia maji ya visima ambayo nayo sio salama pia kwa sababu visima havijapimwa kuthibitisha ubora wake kama sheria zinavyotaka. Matumizi ya maji yasiyo safi na salama, yamekuwa yakisababisha magonjwa mengi yakiwamo UTI, ngozi na kadhalika.
Diwani wa Kata Pangani, Augustine Mdachi akizungumza baada ya ziara ya Kamati ya siasa Chama cha Mapinduzi Kata Pangani, waliyoifanya leo anasema kero ya maji sasa inakwenda kuwa historia kutokana na ukweli kuwa mradi huo ni mkubwa na utakiwa uwe umekamilika kabla ya Julai mwaka huu.
Alipoulizwa kama wananchi wa mitaa yote watamnufaika na mradi huo, Diwani Mdachi anasema anaendelea kuwasiliana na watalaam pamoja na mamlaka nyinginezo kuhakikisha mradi unawanufaisha wote kwani lengo ni kuona kero ya maji inakwisha.
Mradi huo wa tanki la maji litakalokuwa na ujazo wa lita milioni tano unatekelezwa na mkandarasi CDEIC & HAINAN JOINT VENTURE chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ambapo wakazi zaidi ya 60,000 watahudumiwa.
Baadhi ya wananchi wakizungumza wakati Kamati ya siasa ilipokwenda kukagua miradi ya maendeleo kata ya Pangani, walisema wamekuwa wakitumia maji ya visimani yasiyo salama kiafya.
Grace Haule na Jane Mligwa wanasema wamekuwa wakitumia muda mwingi nyakati za usiku na mchana kwa ajili ya kutafuta huduma hiyo badala ya kupumzika na waume zao. "Visima vyenyewe licha ya kwamba sio salama, lakini vimekuwa mbali kuvifikia, tumekuwa tukiacha kulala na waume zetu kitandani kwenda kusaka maji, mradi huu utakuwa ni mkombozi mkubwa "alifafanua Grace.
Lengo la Serikali ni kumtua ndoo mama kichwani, hivyo ni wajibu wake kusimamia kero iliyopo ili wananchi wasambaziwe maji majumbani. Juhudi zinaendelea kufanyika ili wananchi waweze kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇