Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anamuapisha leo aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi kufuatia uteuzi alioufanya jana, Machi 14, 2022.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Zuhura Yunus, ilisema Rais Samia atamuapisha Polepole katika hafla itakayofanyika katika Viwanja vya Ikulu, Chamwino Jijini Dodoma, kuanzia saa 4 asubuhi.
Kabla ya uteuzi Polepole mbali na kuwa Mbunge wa Kuteuliwa wa Bunge tangu Novemba 29, 2020 alikuwa amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo na baadaye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Idara ya Itikadi na Uenezi.
Kufuatia uteuzi huo, Polepole anachukua nafasi ya aliyekuwa Balozi katika Nchi hiyo ya Malawi Balozi Benedict Martin Mashiba ambaye aliapishwa Agosti Mosi, 2017, naye akichukua nafasi ya Victoria Richard Mwakasege ambaye alistaafu.
Taarifa imesema pamoja na Polepole, Rais Samia amemteua pia Waziri Kiongozi mstaafu Shamsi Vuai Nahodha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Ibara ya 67(2) (g) ikisomwa pamoja na Ibara ya 71(1)(a).
Wengine walioteuliwa na Rais Samia katika uteuzi huo alioufanya jana, ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Waziri Kindamba Waziri ambaye amemteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe kuchukua nafasi ya Mhandisi Marwa Mwita Rubirya ambaye amestaafu kwa umri.
Amewateua pia Balozi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (Mstaafu) Ernest Jumbe Mangu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Bandari (TPA) na Meja Jenerali John Mbungo, Mkurugenzi Mstaafu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Meli Tanzania (MSCL).
Aidha Rais amemteua aliyekuwa Mkurugenzi Mstaafu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Peter Ulanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Nehemia Mchechu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo aliwahi kutumikia Shirika hilo huko nyuma kwa nafasi hiyo hiyo ya Mkurugenzi Mkuu na anachukua nafasi ya Dk. Maulid Banyani ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Humphrey Polepole
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇