Baadhi ya wananchi wakiwa katika mkutano na Mkuu wa Wilaya Kibaha Mjini, Sara Msafiri
Na Dismas Lyassa, Kibaha
"WANANCHI wote wa mitaa ya Mkombozi, Lumumba na Kidimu katika Kata ya Pangani, Halmashauri ya Mji Kibaha, mkoani Pwani nyinyi ni wavamizi wa eneo hili mnaloishi. Kwa maana hiyo mnatakiwa kulipia Tsh2500 kwa mita za mraba ili muweze kupimiwa na kurasimishwa. Kama mtu hawezi kulipia aondoke, atafute ambako atanunua bei rahisi," ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mjini, Mkoani Pwani Sara Msafiri aliyoitoa jana katika mkutano wake na wananchi
Katika eneo hilo kuna nyumba zaidi 8000, zenye wakazi zaidi ya 32,000 ambao sasa wametakiwa kuondoka kama watashindwa kulipia kiasi hicho cha fedha.
“Tafsiri yake ni kuwa kama mtu ana 20 kwa ishirini anapaswa kulipia 1milioni. Kiasi hiki kama huwezi kulipa tafuta eneo lenye bei rahisi,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Mitamba ni mradi uliokuwa chini ya Wizara ya Mifugo, ambao kwa miaka mingi umekufa hivyo kusababisha wananchi kuishi maeneo hayo huku wakigombana na Serikali ikiwataka waishi lakini wasipande mazao ya muda mrefu. Ni mwaka 2012 ndipo Serikali ilipotangaza kuwa eneo hilo sasa wananchi wameruhusiwa kuishi kwa maelezo kuwa halmashauri inaendelea na utaratibu za kuangalia namna ya kuwarasimishia na kuwapimia ili wakae katika makazi ya kisasa.
Maagizo ya Waziri Lukuvi na kinachoendelea
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Pangani Julai 15 mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri aajipange kuwapimia na kuwarasimishia wananchi hao wanaoishi Mitaa ya Mkombozi, Lumumba na Kidimu kwa gharama ya Tsh150,000.
Hata hivyo tofauti na kauli ya Lukuvi, sasa wananchi wameagizwa na Mkuu wa Wilaya Sara Msafiri walipie maeneo hayo upya ambayo wamekuwa wakishi kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
“Suala hili la kuwauzia maeneo mnayoishi limeidhinishwa na Madiwani hawa,” alisema huku akiwaonyesha madiwani aliongozana nao.
Ofisi ya Waziri mkuu, Takukuru yaombwa kuchunguza walioruhusu wananchi kutozwa Tsh2500 kwa mita za mraba
Baadhi ya wananchi wanaomba ofisi ya Waziri mkuu au Takukuru kufuatilia kwa ukaribu mchakato wa mpango wa upimaji katika Kata Pangani na namna gharama zilivyowekwa wakisema una hafuru mbaya.
“Inakuwaje wananchi hatukushirikishwa awali ili kutoa maoni juu ya utaratibu unaofaa wa kutumikilishia? Inakuwaje leo tunashtukizwa…fedha tutapata wapi,” alihoji mwananchi wa Kidimu, Amisi Hugo.
Baadhi ya wananchi wameshauri Serikali kuachana na wananchi wenye makazi, badala yake kama ni kuchukua ichukue maeneo makubwa yaliyo ya wazi kwa mazungumzo maalum ili kutumika kwa ajili ya huduma za jamii kama shule, vituo vya afya nk.
Eneo linalotakiwa kupimwa
Wakili maarufu Joseph Assenga ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Mkombozi anasema awali Wizara ya Maendeleo ya Mifugo kupigitia Livestock Multiplication Unit almaarufu Mitamba walimiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 4,000.
Eneo hilo baada ya kuvamiwa na wananchi, Mitamba ilitoa eneo la ukubwa wa ekari 2963 kwa wananchi ambao walianzisha Mitaa ya Kidimu, Lumumba na baadaye Mkombozi. Eneo hili lilitolewa rasmi mnano mwaka 2012 na moja kati ya ushahidi kulithibitisha hilo ni nyaraka rasmi za Bunge (Hansard).
Baada ya kutoa ekari 2,963 Mitamba walibaki na ekari 1,037 ambazo watu wamekuwa wakivamia siku za hivi karibuni. Hizo ekari 2,963 walikabidhiwa wananchi kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha ili zipangwe, zipimwe na kumilikishwa kwa hati.
Ni migogoro badala ya kupima
Tangu mwaka 2013 kupitia Mkurugenzi wa wakati huo Jenifa Christian Omollo Halmashauri ilijaribu kupima lakini ilishindikana ama kwa sababu ya ukosefu wa fedha ama masharti kandamizi ya upimaji ikiwemo sera ya nusu kwa nusu iliyopangwa na halmashauri.
Baadaye wataalamu wa Halmashauri waliandika Andiko la Kitaalamu na kuliwasilisha Wizarani. Matokeo ya andishi hilo la kitaalamu Halmashauri ya Mji Kibaha ilipata mkopo usiokuwa na riba kutoka Wizara ya Fedha (HAZINA) kiasi cha Bilioni 1.5 kwa ajili ya kupima na kumilikisha viwanja 20,000 katika mitaa mitatu ya Kidimu, Mkombozi na Lumumba ambapo Mtaa wa Mkombozi (ukijumuisha Kidimu) vitapimwa viwanja 11,000 kwa kiasi cha milioni 880 na Lumumba viwanja 9,000 kwa gharama ya milioni 720.
Assenga anaungana na wananchi wengine wengi wa mitaa hiyo ambao wanapinga hoja ya kuwatoza wananchi gharama ya 2,500 kwa kila mita moja ya mraba au milioni kwa kila 20 moja (mita za mraba 400).
Baadhi ya wananchi akiwamo Jumanne Ali wanahoji “Kwanini kila kiongozi anapokuja kuzungumza na wananchi wa maeneo haya anakuja kwa jazba au kama anaenda kuongea na wafungwa watukutu kwenye gereza la maweni pale Tanga”.
Mwananchi mwingine Khaflan Said anasema “Binafsi nilikopa fedha Benki nikajenga, na pia naamini hata ninyi wenzangu huenda mlikopa au kudunduliza kwenye vibaba mpaka mkatimiza malengo ya ujenzi. Nyumba hizi kama tukishindwa kulipa tukavunjiwa tutakwenda kuishi wapi?”.
Tangu kumalizika mkutano huo kumekuwa na makundi ya wananchi wakijadili hatma ya maisha yao. Wananchi sasa wanamuomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia suala hili ili wapimiwe kwa utaratibu wa kawaida unaofahamika wa Tsh150,000 na kwamba wale wenye maeneo makubwa ndio wanaweza kuchukuliwa ili yatumike kwa ajili ya huduma za jamii.
Mwisho
Sisi wananchi wa kata ya Pangani kibaha tunaomba viongozi wetu watusaidia suruhisho sahihi na kuweza kulipa pesa ya upimaji kama wizara ilivyopanga kwa tanzania nzima.
ReplyDeletena sio hii waliokuja nayo mkurugenzi na Dc ya kututa wananchi tulipe 2500 kwa square meter 1.
Viongozi wetu tunaomba sana mtusaidie
Huu ni uonevu kwa wananchi. Serikali ichukue hatua haraka na irudishe utaratibu kama yalivyo maeneo mengine.
ReplyDeleteKWA MTIRIRIKO HUU WA USHAHIDI WA WANANCHI NA UONGOZI WA ALMSHAURI YA KIBAHA....INAONYESHA DHAHIRI...VIONGOZI WA JUU (MKUU WA MKOA,WIZARA YA ARDHI,OFISI YA RAISI)..KULIANGALIA KWA JICHO LA UMAKINI....INALETA TAFSIRI MBAYA YA UKANDAMIZAJI AU TAFSIRI YA SERIKALI KUSHINDWA KUWAJIBIKA NA MAONI YA WANANCHI WAKE.....VIONGOZI FUATILIENI HILI JAMBO KUEPUSHA MIGONGANO ISIYO YA LAZIMA KUFIKIA KUHARIBU UTULIVU WA WALIPA KODI WENU (WANANCHI)
ReplyDelete