Na Maalum, Ofisi ya AG
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeanda mafunzo maalumu ya siku tano ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Makamu Wenyeviti wa Kamati, na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, ambayo yameanza jana, katika Ofisi Ndogo ya Bunge Mjini Zanzibari.
Katika mafunzo hayo ambayo Mgeni rasmi alikuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Aksoni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Eliezer Feleshi ( Mb) ni miongoni mwa viongozi wanaoshiriki mafunzo hayo akiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge.
Katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo, mada iliyowasilishwa kwa washiriki ilihusu madaraka, majukumu, mipaka ya utendaji kazi, uzoefu na changamoto na uendeshaji wa Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati ya Uongozi.
Mada hiyo iliwasilishwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamburi ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda, huku wadadisi wa mada wakiwa ni Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Pandu Amir Kificho na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pius Msekwa.
Aidha mada nyingine iliyowasilishwa katika siku ya kwanza ni pamoja na Bima ya Maisha iliyowasilishwa na Shirika la Bima la Taifa ( NIC).
Kwa mujibu wa ratiba ya mafunzo hayo, leo Jumanne, Washiriki hao wataelimishwa na kujengewa uwezo kuhusu; uzoefu, changaoto na mbinu za uendeshaji bora wa vikao vya Bunge la Vyama Vingi vya Siasa.
Mada hiyo itawasilishwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pius Msekwa, huku wadadisi wa mada hiyo wakiwa ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda na Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Kificho.
Aidha mada nyingine itakayowasilishwa na kujadiliwa wakati Mafunzo hayo ni juu ya Uratibu wa shughuli za Bunge na Serikali; uzoefu na changamoto.
Mada hii itawasilishwa na Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ( Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora).
Washiriki wa Mafunzo hayo pia watajengewa uwezo kuhusu misingi ya uongozi na utawala bora, mada itakayotolewa na Mtaalamu kutoka Uongozi Institute.
Viongozi hao wa Bunge pia watajengewa uwezo kuhusu masuala ya Diplomasia, Itifaki, Miiko na masuala muhimu yanayojenga Haiba ya Viongozi. Mada hii itawasilishwa na Mtaalamu kutoka Chuo cha Diplomasia.
Vilevile Viongozi hao wataelimishwa kuhusu huduma za Bima ya Afya kwa wabunge, uzoefu, mafanikio na changamoto itakakowasilishwa na Mtaalamu kutoka Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya ( NHIF).
Mada nyingine itakayotolewa itahusu Dhima ya mgawanyo wa madaraka na namna ya kudhibiti muingiliano wa madaraka ya Mihimili ya Dola. Mada hii itawasilishwa na Mhe, Jumanne Sagini ( Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani. Mafunzo haya yanatarajiwa kuhitimishwa Februari 25/2022.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇