Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Elihuruma Mabelya(Kushoto) wakati wa tukio la Makabidhiano ya madarasa ya Sekondari 157 yaliyojengwa katika Wilaya hiyo.Fedha za ujenzi wa madarasa hayo umetokana na fedha zaidi ya Sh.bilioni tatu ambazo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni mkakati wake wa kutatua changamoto ya upungufu wa madarasa katika Shule sa sekondari
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam Jokate Mwegelo ameshiriki katika hafla ya makabidhiano ya Madarasa mapya 157 yaliyojengwa katika Shule 24 za Sekondari iliyofanyika Januari 3, 2022 katika Shule mpya ya Sekondari Dovya iliyopo Kata ya Chamazi wilayani humo.
Katika hafla hiyo Jokate amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha fedha Sh.Bilioni 3.14 za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa, na mapambano dhidi ya UVIKO 19 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa madarasa hayo.
Ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ulioanza Novemba 1, mwaka 2021 na kukamilika Disemba 31, 2021 na kukamilika na kukabidhiwa kwa madarasa hayo vitakavyoondoa changamoto ya madarasa kwa muhula wa masomo wa mwaka 2022.
Akizungumza leo wakati wa tukio la Makabidhiano ya madarasa hayo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Jokate Mwegelo ametumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo Temeke inamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo zimekwenda kutatua changamoto ya masomo ,hivyo msimu wa masomo wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato Cha kwanza wote watakwenda shuleni.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika miradi inayotekelezwa na serikali, ili kuwafanya kutambua matumizi ya mapato yanayokusanywa na halmashauri yao kwa maendeleo ya Temeke, huku akitumia fursa hiyo kuwaomba wazazi na walezi kuwahimiza watoto wao wafike shule kwa wakati, kwa sababu madarasa hayo yamejengwa kuimarisha elimu ya sekondari nchini.
“Miradi yote ya maendeleo lazima tushirikishe Wananchi ili wajionee 'laivu' bila chenga, tutaendelea kuwashirikisha Wananchi kuanzia miradi inapoanzishwa, inapoendelea, inapokamilika, mapato, matumizi na hata kwenye uzinduzi kuwaomba wawepo ili kuona kwa vitendo na sio kusimulia tu” amesema Jokate
Aidha ametoa mwito kwa viongozi wa bodi za shule za Sekondari kuendelea kukaa vikao kazi muhimu, ili kuendelea kujadili namna bora ya usimamizi wa shule, kuinua maendeleo ya elimu, na kukuza viwango vya ufaulu wa wanafunzi ili kuipaisha Wilaya ya Temeke katika ramani bora ya elimu nchini.
Ameongeza ni vema akatoa shukrani kwa Meya, Naibu Meya , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ,Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano mkubwa ambao wameutoa wakati wote wa kutekeleza miradi ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa madarasa hayo huku akiwashukuru pia viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwa usimamizi wao wa kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇