Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akikagua Daraja la mto Ipeja liliyojengwa kwa fedha za tozo kwa shilingi milioni 485 kushoto ni mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude.
SALVATORY NTANDU
KISHAPU
Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga imeishauri serikali kuongeza usimamizi katika miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za tozo za miamala ya simu ili ziweze kuleta tija ikiwa ni pamoja na kutatua kero za wananchi ikiwemo za kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kijamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa wakati akikagua ujenzi wa kituo cha afya Negezi katika kata ya Ukenyenge kilichopatiwa shilingi milioni 250 na Rais Samia Suluhu Hasani ili kusogeza huduma za matibabu kwa wananchi.
“Wajumbe wa kamati ya siasa mkoa, tumekagua ujenzi wa majengo ya kituo hiki na imeridhika na ujenzi wake,tunachoshauri serikali iongeze usimamizi katika mradi huu ili ukamilike kwa wakati na uweze kuleta matokeo chanya kwa kusogeza huduma za afya kwa wananchi karibu na maeneo yao,”alisema Mlowa.
Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu alitoa fedha hizo ili zitatue kero ya afya iliyokuwa ikisababisha wakazi wa kata ya ukenyenge kusafiri umbali mrefu na kufuata huduma za afya katika kata za jirani hivyo ni budi serikali ikaongeza usimamizi wa fedha hizo ili majengo ya kituo hicho yakamilike kwa wakati kama inavyotakiwa.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo cha afya Ukenyenge,muuguzi mfawidhi wa Zahanati ya kijiji cha Negezi Agness Wiliam alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 85 na utakamilika kwa wakati ili uwe kutoa huduma kwa wananchi wa vijiji vine vinavyounda kata ya Ukenyenge.
“Kituo hiki kitasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Zahanati ya ukenyenge ambayo kwa mwezi tunatoa huduma kwa wagonjwa wa nje 500 wajawazito wanaojifungua 35 hadi 40 na ambao wanahitaji huduma za upasuaji hulazimika kupewa rufaa na kusafiri umbali wa kilomita 20 kwenda katika makao makuu ya wilaya ili kupata huduma hiyo,”alisema Wiliam.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude aliahidi kupokea maelekezo ya kamati hiyo kwaajili ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kuongeza usimamizi katika ujenzi wa majengo yote yanayoendelea kujengwa ili fedha na tathamani ya mradi visitofautiane.
“Sisi kama watekelezaji wa ilani tunawaahidi kufanyia kazi maelekezo ya kamati ili wananchi wetu waondokane na kero hizo ambazo Rais Samia Suluhu Hasan ameamua kuzitatua kupitia fedha za tozo,”alisema Mkude.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇