LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 15, 2021

MKUTANO MKUU WA TAHOSSA KUANZA LEO, KUJADILI MAMBO KADHAA IKIWEMO MAFANIKIO KATIKA ELIMU IKIWEMO UJENZI WA SHULE NA MAELFU YA MADARASA CHINI YA UONGOZI WA RAIS SAMIA

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mkutano wa Mkuu wa 16 wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania, utakaofanyika kwa siku tatu, unaanza leo Jumatano, Disemba 15, 2021, katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam, huku ukitarajiwa kuhudhuriwa na Wakuu hao zaidi ya 5,000.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA), Titus Jumanne amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo utajadili mafanikio  mbali mbali yaliyopatikana katika sekta ya Elimu katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwemo ujenzi wa shule na maelfu ya madarasa mapya.

Mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka unalenga kuwaleta pamoja Wakuu hao wa shule za Sekondari ili kubadilishana mawazo, uzoefu, changamoto, mafanikio na utekelezaji wa sera na mipango inayotolewa na serikali.

Katibu Mkuu huyo wa TAHOSSA ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha kwaajili ya ujenzi wa shule moja ya wasichana kwa mikoa 10 hali ambayo alisema itasaidia kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu watoto wa kike kwenda shule.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imejitahidi kuhakikisha ufaulu kwenye Elimu ya Msingi na Sekondari unaongezeka kwa kuweka miundombinu na walimu wa kutosha yote hayo ikiwa ni kuboresha elimu.

Katibu Mkuu huyo ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia kwa kupeleka Sh. bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 214 za Sekondari ambazo zitajengwa kwenye majimbo yote nchini ambapo Rais pia aliagiza Sh. Bilioni 30 zitumike kujenga shule mpya za Wasichana pekee ambapo kwenye mikoa 10 itajengwa shule moja moja ya wasichana.

“Pia Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia imeagiza ujenzi wa shule 1,000 za Sekondari katika Kata ambazo hazina shule za Sekondari, hii haijapata kutokea na serikali ya awamu ya sita inastahili pongezi za dhati kabisa,” alisema Jumanne.

Katibu Mkuu huyo wa TAHOSSA amesema Mkutano huo pia utaambatana na matukio mbalimbali ikiwemo utoaji wa zawadi mbalimbali kwa Shule, Walimu na Wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages