LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 29, 2021

JUMLA YA MAKOSA 1,795 YALIFANYWA NA WALIMU KATIKA YA 2020-21, IKIWEMO KUJIHUSISHA NA MAPENZI, KUGUSHI VYETI

Na CCM Blog, Dodoma
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Nchini imesema  katika kipindi cha mwaka jana hadi mwaka huu wa 2021, jumla ya makosa 1,795 yalifanywa na Walimu, huku walimu hao wakifanya makosa 184 kati ya mwezi Julai hadi Septemba, 2021.

Imeelea kuwa makosa hayo 1,795 yaliyofanywa na Walimu yalihusu utoro, kugushi vyeti, uhusiano wa kimapenzi, ukaidi na ulevi huku ikisisitizwa Walimu kuingatia maadili katika utumishi wao kwa kuwa kazi ya Ualimu haiwei kufanyika kwa ufanisi bila kuzingatiwa maadili.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Willy Komba alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya hali ya maadili ya kazi ya Ualimu hadi kufikia mwaka huu wa 2021 ambao unafikia tamati keshokutwa..

Prof. Komba amesema kuwa elimu kwa ujumla wake imejikita katika maadili hivyo, bila maadili hakuna elimu kwani inawezekana kwenda shule hadi elimu ya juu lakini kama mtu hana maadili atakuwa amesoma lakini hajaelimika.

“Elimu inaenda sambamba na maadili, tunachoona kinaendelea madarasani, Walimu wetu wengi wanajikita zaidi katika kutoa maarifa kulingana na somo analofundisha lakini suala la maadili wamewaachia viongozi na walimu wenye vipindi vya dini, hii sio sawa kwani kazi ya ualimu ikiweka maadili pembeni inakuwa haijakamilika”, alisema Prof. Komba.

Amesisitiza kuwa, adhabu zote zinazotolewa kwa Walimu zinaendana na Kanuni na Tararibu za Tume na kwamba Tume hiyo inajitahidi kutenda haki hivyo, kwa wale ambao hawaridhiki na maamuzi wanaruhusiwa kukata rufaa kwa Kamati ya Nidhamu ya Wilaya, Tume pamoja na kukata rufaa kwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika hatua nyingine, Prof. Komba amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuwapandisha madaraja Walimu 126,346 pamoja na kurekebisha mishahara yao kwa wakati.

Vile vile amewashukuru Walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutoa elimu na kusimamia miradi mbalimbali ya sekta ya elimu kwani pamoja na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo bado viwango vya ufaulu vinaongezeka.


Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Willy Komba akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu maadili ya kazi ya Ualimu.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages