Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, jana Jumamosi, Novemba 27, 2021, ametangaza uteuzi wa viongozi mbali mbali akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Balozi Ombeni Sefue.
Taarifa ya Ikulu ilimesema katika Uteuzi huo Rais amemteua Balozi Ombeni Sefue, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) kuchukua nafasi ya Dk. Stergomena Tax ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Jafar Haniu, uteuzi huo wa Balozi Sefue ulianza Novemba 24, 2021.
Pia Rais amemteua Mwenyekiti na Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya Uwakili ya FMD Legal Consultants and Advocates Balozi Mathias Meinrad Chikawe, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanzania and Italian Petroleum Refining Company Limited (TIPER) ambaye naye uteuzi wake ni tangu Novemba 24, 2021.
Taarifa imesema wengine walioteuliwa katika uteuzi huo ni Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe, Katibu Mkuu Mstaafu – TAMISEMI kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambaye uteuzi wake ulianza Novemba 16, 2021 na Prof. Ephata Elikana Kaaya kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Kilimanjaro (KCMUCo), Kilimanjaro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Saratani Ocean Road ambaye yeye uteuzi wake ulianza Novemba 15, 2021.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kazini
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇