*****************
Na. John Mapepele, WUSM.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na michezo. Mhe, Innocent Bashungwa amesema Serikali imeshakamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya kuanza mashindano ya Mataifa ya Afrika ya Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu (CANAF) yanayotarajiwa kuanza kesho jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye Mkutano wa Waandishi wa Habari leo, Novemba 26, 2021 akiwa ameambatana na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulamavu nchini, Moses Mabula, Mhe. Bashungwa amesema Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mashindano hayo kutokana na uzoefu na umakini katika kuandaa mashindano ya kimataifa ya michezo.
“Ndugu zangu Waandishi tunafurahi kuona kuwa nchi yetu imeendelea kuratibu mashindano mengi ya kimataifa, hii inatokana na uzoefu katika nyanja mbalimbali ya kuandaa mashindano haya”. Amefafanua Mhe. Bashungwa.
Aidha, Mhe. Bashunga ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais kwa kutoa shilingi milioni 150 jana ili zisaidie kwenye maandalizi ya mashindano ya Timu ya Soka ya Taifa ya Walemavu ya Tanzania “Tembo Warriors”.
Pia amesema kwenye mashindano haya Tanzania imechukua tahadhari zote za ugonjwa wa Uviko-19.
Naye Mabula ameishukuru serikali kwa kuisaidia timu hiyo na kuihakikishia Serikali kufanya vizuri katika mashindano hayo ambapo amesema kwa mara ya kwanza mashindano haya yatahusisha kufuzu kuelekea kombe la dunia tofauti na awali.
Wakati huo huo, Mhe. Bashungwa amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuitangaza tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani. Kufuatia hatua hii muhimu.Ametoa wito kwa wapenzi, wadau na asasi mbalimbali za Kiswahili hapa nchini kuongeza mbinu za Kisasa za kukitumia na kukitangaza Kiswahili duniani.
“Tuhamasishe wadau wa fani nyingine kama vile za Uhandisi, Sheria na Habari ili wakipende Kiswahili na kukitumia katika shughuli zao”. Ameongeza Mhe. Bashungwa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇