Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Serikali ya Shirikisho la Ujerumani imeahidi mwezi ujao itaanzisha majadiliano na Serikali ya Tanzania kuhusu maeneo ambayo inaweza kusaidia kutokana na athari za UVIKO 19.
Taarifa iliyotolewa jioni hii na Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema ahadi hiyo imetolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati Rais Samia Suluhu Hassan aliookuwa akizungumza naye kwa njia ya simu, leo.
Imesema mbali na ahadihiyo Merkel amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kupambana na UVIKO 19 na kuahidi pia kuunga mkono jitahada hizo kwa kutoa msaada wa chanjo za kukabiliana na ugonjwa huo.
"Katika mazungumzo hayo, Merkel amempongeza Rais Samia kwa kushika hatamu ya Urais nchini Tanzania na kumpa pole kufuatia kifo cha Aliyekuwa Rais wa Awamu ya tano Hayati Dk. John Pombe Magufuli", imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema katika mazungumzo hayo Markel amempongeza pia Rais Samia kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ambapo ameahidi kuwashawishi wafanyabiashara wa Ujerumani na watalii kutembelea na kuwekeza nchini Tanzania.
"Kwa upande wake Rais Samia amemshukuru Merkel kwa ushirikiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Rais Samia amempongeza Merkel kwa kumaliza kipindi chake cha uongozi akiwa ni kiongozi wa kisiasa mwanamke aliyeongoza muda mrefu ndani ya Chama chake cha CDU na ndani ya Jumuiya ya Ulaya", imesema Taarifa hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwa njia ya simu na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Sept 01, 2021. Picha na Ikulu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇