Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma mpya ya WEKEZA Akaunti uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Meneja Mwandamizi Idara ya Bidhaa, Janet Rwegasila na Mkuu wa Idara ya Bidhaa Benki ya NMB, Aloyse Maro.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Benki ya NMB leo imezindua akaunti mpya kabisa inayoenda kwa jina la Wekeza itakayomuwezesha mteja kuweka akiba ya muda mrefu na kupata riba kubwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi amesema kuwa uzinduzi wa jambo hilo kubwa katika kipindi hiki ni kuwakumbusha watanzania na wateja wa NMB kujitunzia akiba kwa Maisha ya baadae.
"Akaunti ya wekeza ni ya kwanza na ya aina yake kuwahi kutokea nchini Tanzania ambapo mteja anajitunzia fedha zake kuanzia 250,000 na kupata riba kubwa mpaka asilimia 12 kulingana miaka ambayo mteja anakusudia kuwekeza akiba yake,"amesema Mponzi.
"Sio hicho tuu, mteja atakapojiandikisha kwenye akaunti ya Wekeza atapata bima ya maisha bure endapo atafariki au kupata ulemavu wa kudumu atalipwa mara mbili ya akiba /uwekezaji wake. Kima cha chini kwa mteja kupata bima hii ni Shilingi milioni 2 mpaka Shilingi milioni 50."
Amesema kuwa muda wa kutunza akiba hiyo ni kati ya miaka 6 mpaka 20 na kwamba riba hulipwa mara mbili kwa mwaka (Juni na Desemba). Mteja atakuwa na uwezo wa kuongeza akiba kupitia matawi ya NMB, Mawakala wa NMB na NMB Mkononi.
"Hii maana yake ni kuwa, sisi kama benki iliyo salama zaidi nchini na kinara wa ubunifu katika utoaji wa huduma za benki, tunaendelea kuwekeza kimkakati kwenye teknolojia na mtandao wa matawi yetu huku tukiimarisha uwezo wetu wa kuihudumia jamii. Lengo likiwa kuwawezesha wateja kuimarisha zaidi kipato na uchumi wao."
Aidha, amesema kuwa benki hiyo inatabia ya kubuni bidhaa zinazowasaidia wateja kuokoa muda na fedha na kutumia teknolojia ya kisasa zaidi kufanya hivyo. Inahitaji kila mtu kuzisimamia fedha zake akiwa na uelewa wa kutosha. Wateja watakao ruhusiwa ni wale wenye akaunti binafsi.
NMB imepanua wigo wa akaunti zake binafsi ili kuwawezesha wateja wetu kuwa na amani zaidi katika kusimamia fedha zao kwani akaunti hii ni kama kibubu chenye faida nyingi sana ambazo zitamsaidia mteja kuwa na tabia ya kujiwekea akiba kwa matumizi yenye malengo.
Amesema benki ya NMB imeangalia soko la Tanzania taarifa za wateja wake na kuona kuwa watu wengi hawana tabia ya kuweka akiba kwa muda mrefu, hivyo imeona ipo haja ya kuwaletea akaunti ambayo itawasaidia kuweka akiba.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇