Ikulu, Chamwino Dodoma, leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 13Agosti, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya El Sewedy Electric kutoka nchini Misri, Mhandisi Ahmed El Sewedy,Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Raais, Ikulu jijini Dodoma Jaffar Haniu, imesema, katika mazungumzo hayo, Mhandisi El Sewedy amemfahamisha Mhe. Rais Samia kuwa kampuni yake mbali na kuwa miongoni mwa kampuni zinazojenga mradi wa kuzalisha umeme katika Bwala la Mwalimu Nyerere, pia imewekeza katika miradi mingine na kutarajia kuwekeza zaidi hapa nchini.
Mhandisi El Sewedy amesema Kampuni yake inajenga mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 2115 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere na pia katika eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam, Kampuni yake imejenga kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme, transfoma, vifaa vya kuzuia nyaya za umeme zisilete hitilafu na mita za umeme, ambacho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi mwezi Disemba mwaka huu.
Taarifa hiyo imesema, Mhandisi huyo amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuwekwa na Serikali, wameamua kuunga mkono na kuwekeza zaidi kwa kujenga eneo la viwanda lenye ukubwa wa mita za mraba milioni mbili ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha mbolea na pia anatarajia kuwekeza katika ujenzi wa reli ya kisasa, na katika kipindi cha miaka mwili atahamasisha Kampuni takriban 50 kutoka Misri kuja kuwekeza hapa nchini.
Kwa upande wake, Rais Samia amemshukuru Mhandisi El Sewedyna kumuhakikishia kuwa Serikali itampa ushirikiano katika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo kwa muda muafaka na kwamba ujenzi wa eneo maalum la viwanda litasaidia kuchangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa ajira na ujuzi.
Rais Samia amemjulisha Mhandisi huyo kuwa kwa sasa Tanzania inapitia sheria na sera zake mbalimbali ili kujenga mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mhandisi Ahmed El Sewedy Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya El Sewedy Electric ya Nchini Misri, Ikulu Chamwino Jijini Dodoma leo Agosti 13, 2021. (Picha na Ikulu)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇