Kaimu Mkurugenzi wa Urasimishaji Ardhi na Biashara wa Mkurabita, Jane Lyimo akizungumza. |
Wafanyabiashara mbalimbali jijini Dar es Salaam wanaalikwa kufaidi mafunzo hayo. |
WAFANYABIASHARA takribani 1000 wanatarajia kuanza kunufaika na mafunzo ya urasimishaji Ardhi na Biashara yanayotarajiwa kutolewa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA). Mafunzo hayo yanatarajiwa kutolewa kwa siku nne kwa Wafanyabiashara wa kata saba za Jiji la Dar es Salaam; ambazo ni pamoja na kata za Tabata, Liwiti, Segerea, Kisukuru, Kinyerezi, Bonyokwa na Zingiziwa.
Akizungumzia zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Urasimishaji Ardhi na Biashara wa Mkurabita, Jane Lyimo, alisema miongoni mwa mambo watakayonufaika nayo washiriki wa mafunzo hayo ni pamoja na upatikanaji wa fursa za mikopo kwa wafanyabiashara wanaotaka kukuza biashara zao pamoja na mitaji kwa walio katika hatua za awali.
Bi. Lyimo alisema mafunzo hayo yatakayoanza kesho hadi Alhamisi ijayo, yatafanyika katika vituo viwili vya Barakuda na Zingiziwa. Akifafanua zaidi alisema miongoni mwa mambo yatakayofundishwa ni utunzaji wa kumbukumbu muhimu za biashara, zana na faida ya kituo jumuishi cha urasimishaji na uendelezaji biashara maarufu ‘one stop center’ kinachotarajiwa kuanzishwa jijini humo maeneo ya Mnazimmoja mwishoni mwa Julai, 2021, upatikanaji wa leseni za biashara na faida zakena huduma za mlipakodi yaani taratibu za ulipaji na viwango halisi vya kodi.
“Pia washiriki watanufaika kwa mafunzo kuhusu huduma za benki na utaratibu wa upataji huduma za mikopo, huduma za SIDO (Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo) na huduma za mifuko ya pensheni...Wafanyabaishara watumie fursa hii kupata elimu kuhusu biashara na mitaji kwa ajili ya kukuza biashara na kutatua changamoto wanazokutana nazo kuhusu kodi…” Alisema Bi. Lyimo.
Alisema mafunzo hayo yanayotarajiwa kuanza keshokutwa katika Kituo cha Barakuda, yatatolewa na taasisi mbalimbali wadau wa biashara ikiwamo Benki ya NMB itakayotoa mada na huduma za kibenki zikiwamo za kufungua akaunti za ‘chapchap’.
Taasisi nyingine zitakazoshiriki kutoa mafunzo na huduma jumuishi ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hususan masuala ya biashara na lesni, mfuko wa hifadhi ya jamii wa NSSF. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Sido na Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
“Uwepo wa wadau hao utawawezesha wafanyabiashara kupata huduma zote jumuishi za kibiashara mahali hapo zikiwamo za kupata leseni za biashara, kupata namba ya mlipakodi (TIN) na kusajili majina ya biashara, kampuni na ubia na NMB itawezesha fursa zaidi muhimu za mikopo ili kukuza au kupata mitaji,” alisema Lyimo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇