Serikali inafanya
marekebisho ya sheria ya vyama vya ushirika nchini ili kuhakikisha kuwa
mali na shughuli zote za vyama hivyo zinasimamiwa na wanachama wenyewe.
Lengo la marekebisho
ya sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2013, ni kuhakikisha kwamba vyama vya
ushirika vinajisimamia vyenyewe bila kuingiliwa na viongozi kutoka
serikalini.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda
alibainisha hayo wakati wa siku ya maadhimisho ya siku ya ushirika
duniani iliyofanyika kitaifa mwishoni mwa wiki mkoani Tabora.
Mgeni Rasmi katika
maadhimisho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu ‘Ushirika Pamoja, Tujenge Upya
kwa Ubora na Tija’ alikuwa waziri mkuu Kassim Majaliwa.
“Ushirika
haulazimishwi kwa kuwa si mali ya serikali na kujiunga ni hiari hakuna
mtu anayelazimishwa, mamlaka ya serikali katika ushirika yana mipaka
yake,’’ alisisitiza.
Prof Mkenda aliongeza
kuwa hakuna kiongozi mwenye mamlaka ya kuviagiza vyama vya ushirika
kutoa fedha katika akaunti zao kwa ajili ya matumizi yoyote.
“Ushirika ni hiari na
mali ya wanaushirika, hivyo wanachama wanatakiwa kujua kwamba ni mali
yao, wasimame kidete kusimamia shughuli zao bila kuingiliwa kinyume na
utaratibu na sisi viongozi wa serikali lazima tujue mipaka yetu,’’
alisema na kuongeza:
“Hakuna ruhusa kwa kiongozi yeyote kwenda kuwapangia matumizi ya fedha zao.’’
Hata hivyo Waziri
Mkenda alisema kuwa serikali ina wajibu kwenye ushirika kwa sababu
wanaushirika ni wengi na kuna viongozi wao na pia kuna sheria
inayowatambua.
“Ndani ya serikali
kazi yetu ni kuhakikisha sheria inafuatwa, viongozi wanawajibika kwa
wanaushirika wao na maamuzi yote ya wanaushirika yanafanywa na wanachama
na si kukundi tu cha watu wachache,’’ alisema.
Prof Mkenda aliongeza
kuwa serikali itaendelea kusimamia ushirika kuhakikisha kuwa
unasimamiwa kwa weledi, uwajibikaji na uwazi ili kuhakikisha kuwa watu
wengi wanapenda na kukubali kujiunga na vikundi mbalimbali vya ushirika.
Kila mwaka, siku ya
ushirika duniani huadhimishwa kila siku ya jumamosi ya kwanza ya mwezi
wa saba. Kwa mara ya kwanza siku hii iliadhimishwa chini ya usimamizi wa
umoja wa mataifa mwaka 2005.
Madhumuni ya
maadhimisho haya ni kuongeza uelewa kwa wanaushirika na kuimarisha
mafanikio ya umoja wa kimataifa, uchumi endelevu, usawa na amani kote
duniani.
Siku hii pia ina
lengo la kuendeleza na kutanua ushirikiano baina ya ushirika wa
kimataifa na nchi zingine duniani ikiwemo kushirikisha serikali kwa
ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇