………………………………………………..
Ndugu Wananchi;
Kesho tarehe 18 Julai, mwaka huu, kama mnavyofahamu ni siku ya kupiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Mbunge na madiwani katika Jimbo moja na kata mbili. Uchaguzi huu unahusisha Jimbo la Konde lilipo katika Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa kaskazini Pemba na Kata mbili (2) za Mbagala Kuu, katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Mchemo katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Ndugu Wananchi;
Tume inatumia nafasi hii kuvipongeza Vyama vya Siasa na wagombea waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi huu mdogo, pamoja na wananchi wote wa jimbo na kata zenye Uchaguzi kwa utulivu ulioonyeshwa wakati wote wa kipindi cha Kampeni ambacho kinahitimishwa leo.
Uchaguzi huu mdogo wa kiti cha Ubunge na madiwani utahusisha jumla ya vyama vya siasa 14 vilivyosimamisha wagombea, Wapiga Kura 66,441 na utafanyika katika vituo vya Kupigia Kura 233.
Ndugu Wananchi;
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala, wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia mambo yafuatayo:
- i) Kwa kuwa kesho jumapili tarehe 18, Julai, mwaka huu ni siku ya
Uchaguzi mdogo wa Ubunge na Udiwani katika maeneo tajwa ya uchaguzi, Vyama vya siasa, Wagombea na wafuasi wao hawatakiwi kufanya mikutano ya kampeni zaidi ya saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni ya leo. Baada ya muda huo pia hairuhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera, mavazi nk.
- ii) Upigaji kura utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati
wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
iii) Vituo vya Kupigia Kura vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi
na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni. Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni.
- iv) Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye jimbo na kata husika na wana kadi zao za Mpiga kura. Hata hivyo, Tume kwa kuzingatia
masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.
Mojawapo ya kitambulisho mbadala ambacho mpiga kura anaweza kutumia ni; Pasi ya kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
- v) Mpiga Kura aliyepoteza kadi yake au kadi yake kuharibika ataweza
kuruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala, iwapo tu; atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo katika orodha ya Wapiga Kura katika kituo anachokwenda kupiga Kura. Aidha, majina yake yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yafanane na yale yaliyopo katika kitambulisho mbadala.
- vi) Tume, kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 12A cha Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, watakaopiga kura katika uchaguzi mdogo Jimbo la Konde ni wale tu walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
vii) Kutakuwa na majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura
kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kupiga kura bila usaidizi. Kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo, wataruhusiwa kwenda
vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
viii) Katika vituo vya kupiga kura, Kipaumbele kitatolewa kwa
wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni.
- ix)
Kwa mujibu wa maelekezo yaliyomo katika Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2020 ambayo yaliridhiwa na wahusika vikiwemo vyama vya siasa, Wapiga kura watatakiwa kuondoka vituoni mara tu baada ya kupiga kura. Hivyo, Tume inawashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura.
Vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi wa kesho vinao wajibu na haki ya kuweka mawakala katika vituo vyote vya Kupigia na Kujumlishia Kura. Wajibu wa mawakala hao ni kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea. Pamoja na wajibu huo, Tume inawakumbusha mawakala hao, kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao
vituoni.
Ndugu Wananchi;
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuona hali ya amani na utulivu ambayo imekuwepo kwenye maeneo yenye Uchaguzi hadi hivi sasa inaendelea kuwepo hadi shughuli za uchaguzi zitakapokamilika. Tukumbuke kuwa jukumu la kulinda amani ya nchi yetu ni la kila
mwananchi, vyama vya Siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi. Hivyo, tuepuke kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani.
Vilevile, Tume inavikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wasimamizi
wa uchaguzi kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za
uchaguzi. Iwapo kutakuwa na malalamiko yoyote yatakayojitokeza, taratibu za kisheria na kikanuni zinapaswa kufuatwa katika kuwasilisha na kushughulikia malalamiko hayo kwenye mamlaka zilizowekwa kisheria.
Kwa kumalizia, Tume inatoa rai kwa Wapiga Kura Jimbo la Konde na kata mbili zinazohusika na uchaguzi huu mdogo, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura hapo kesho, ili kuwachagua viongozi wanaowataka.
KUMBUKA KURA YAKO NI SAUTI YAKO,
NENDA UKAPIGE KURA
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇