Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, akizungumza leo jijini Dodoma.
Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza Rais na Menyekiti wa CCM Samia Suluhu Hassan kwa usikivu wake kwa wananchi anaowaongoza na kuamua suala la Tozo za miamala ya simu kutizamwa upya.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amesema, kwa hatua hiyo Rais Samia, ameendelea kuwathibitishia Watanzania na dunia kwa ujumla kuwa ni kiongozi Imara, mzalendo, shupavu na mwenye dhamira ya kweli kwa watu wake anaowagonza ili kuwatoa na kujikwamua na umasikini.
"Chama kinatoa maelekezo kwa Serikali pamoja na kupitia upya tozo hii ya miamala ya simu, lakini pia iandae utaratibu wa kupitia upya sera na sheria ya kodi na kuratibu ubunifu utakaoibua vyanzo vipya vya kodi ili kupunguza mzigo mzito kwa wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa Ibara 18 na Ibara 20 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025", amesema Shaka na kuongeza;
"Chama kinawasisitiza wananchi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuona fahari ya kulipa kodi kwa hiyari na uaminifu kwa maendeleo endelevu ya taifa letu".
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, katika mkutano wake na Waandishi wa Habari, akiwa na Waziri wa Teknolojia ha Habari na Mawasiliano Dk. Faustine Ndugulile, amesema Serikali imesikia maoni na kilio cha wananchi kuhusu tozo hiyo na kuwaomba wawe watulivu wakati jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi.
“Kwa maaneo ambayo wananchi wametoa ushauri na kuelezea namna ambavyo jambo hili linawagusa lakini pia tumepokea maeneo ambayo yanatakiwa kutoa elimu zaidi ili kujenga uelewa wa pamoja ikiwa ni pamoja na viwango vinavyokatwa kwa nayetuma na anayetoa lakini pia kuhusu mantiki ya jambo lenyewe” alisema Mwigulu
Alisema kuwa jambo la tozo za miamala linatekelezwa kupitia sheria iliyopitishwa na Bunge lakini kuna kanuni za utekelezaji zinazo mhusu yeye kama Waziri wa Fedha na Mipango na maeneo mengine yanahusu Wizara ya Teknollojia ya Habari na Mawasiliano ambazo zitajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
Dk. Nchemba alisema kuwa siku ya Jumanne tarehe 20 Julai, 2021 kutakuwa na kikao kilichoitishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kujadili suala hilo na pia kutakuwa na kikao kingine cha Mawaziri wa Wizara zote kuchambua kwa kina suala hilo.
“Lakini Tayari Mheshimiwa Rais naye alishaguswa na jambo hili amesikia maoni ya Watanzania wote na yeye ametolea maelekezo kwamba tuyafanyie kazi maoni hayo.
Nitoe rai kwa Wananchi kuwa watulivu kwenye jambo hili tutaendelea kuelezea na kutoa ufafanuzi kwenye kila maeneo yanayohitaji ufafanuzi na tutachukua hatua kwenye maeneo ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatua ili ujenzi wa taifa letu uweze kuendelea kama ambavyo wananchi wamekuwa na shauku kubwa kuona ujenzi wa Taifa letu unaendelea kwa ajili ya maendeleo ya nchi” Alisema Dk. Nchemba
Dkt. Nchemba aliwaonya wale ambao wana nia mbaya ambao mara zote wapenda kupotosha ama kubadili dhana ya maana halisi ya jambo ambavyo lilikuwa limekusudiwa na kuwataka wasifanye hivyo, kwani mambo haya yana maslahi mapana kwa nchi.
“Haya ni mambo ambayo ni ya kisheria, sheria za nchi zinatakiwa kuheshimiwa, ni mambo ambayo ni ya kikanuni na mambo yanayohitaji uelimishaji tutaendelea kufafanua lakini yale yanayotakiwa kufanyiwa kazi niwaahidi watanzania tutaendelea kuyafanyiakazi kama ambavyo viongozi wetu wakuu wamesema” Alisisitiza Mhe. Nchemba
Alisema tayari aliwapa maelekezo wataalam wa mifumo kuangalia vipengele vya Sheria ya mifumo ya malipo Serikalini pamoja na Sheria ya Mawasiliano ya Mtandao (EPOCA) inayoelezea kuhusu masuala ya miamala kwa njia ya mtandao na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kufikia muafaka wa jambo hilo.
Alitoa Rai kwa watanzania waendelee kumuunga mkono Mhe Rais katika Dira yake ya kuhakikisha anasukuma mbele shughuli za maendeleo ya nchi na ili tuwakomboa na kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Dkt. Faustine Ndugulile alibainisha kuwa Wizara yake pia ambayo inaguswa moja kwa moja na tozo hizo imeendelea kupokea maoni na kuchakata taarifa mbalimbali tangu tozo hiyo ianzishwe na kumwahidi Waziri wa Fedha na Mipango kwamba atampa ushirikiano kuhakikisha kwamba maelekezo yaliyotolewa na viongozi yanatekelezwa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇