Kijana Baraka ambaye anaulemavu wa uziwi kutoona vizuri akiwalisha kuku wake ikiwa ni biashara aliyowezeshwa na Sense International. |
Kijana Baraka ambaye anaulemavu wa uziwi kutoona vizuri akiwalisha kuku wake ikiwa ni biashara aliyowezeshwa na Sense International. |
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Sense International limebainisha kuwa vijana wenye uziwi kutoona wakisaidiwa wanaweza kuwa msaada kwenye familia zao na kupunguza kuwategemea wanafamilia kwa kila kitu. Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Programu kitengo cha Elimu wa Shirika la Sense International, Benjamin Kihwele hivi karibuni alipokuwa akitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuwatambua mapema na kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa uziwi kutoona kwenye Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliyofanyika wilayani Rorya.
Bw. Kihwele alisema Shirika la Sense International licha ya kutoa huduma za utambuzi wa mapema wa hali ya ulemavu uziwi kutoona kwa watoto kuanzia mwaka mmoja hadi miaka mitano katika miradi yao wamekuwa wakiwasaidia kutoa mitaji kwa vijana wajasiliamali wenye changamoto za ulemavu huo mara baada ya kumaliza elimu yao.
Alibainisha kuwa hadi sasa kwa Tanzania takribani vijana viziwi wasioona 36 wamewezeshwa shughuli za uanagenzi baada ya kupewa mafunzo kwa kusaidiana na wanafamilia wao. Alisema vijana wamekuwa wakiwezeshwa shughuli za ujasiliamali wanazozipenda wenyewe na wanazozimudu.
Anasema mara baada ya vijana hao kumaliza elimu yao na kuingia vyuo vya ufundi shirika la Sense International huwawezesha kimtaji vijana ili waweze kuendesha shughuli za ujasiliamali majumbani kwao kwa kuwashirikisha ndugu zao wa karibu (wanafamilia). "Vijana kama hawa wakipata elimu na kuwezeshwa wanaweza kuwa na mchango katika jamii zao, wanaweza kujiingizia kipato na kutoka katika hali ya utegemezi kwa kila kitu," anasema Bw. Kiwele wa Shirika la Sense International.
Mzee Jonathan ni baba mzazi wa kijana Baraka ambaye anaulemavu wa uziwi kutoona vizuri anathibitisha vijana wenye ulemavu huo wakipata elimu na kuwezeshwa wanaweza kujitegemea na hata kusaidia kuongeza kipato katika familia zao. Anasema kijana wake Baraka mara baada ya kumaliza elimu amewezeshwa na Shirika la Sense International shughuli za ujasiliamali na sasa anaendelea kuendesha mradi wa ufugaji kuku wanyama na mayai kwa kushirikiana na wanafamilia.
Kijana Baraka ambaye anaulemavu wa uziwi kutoona vizuri akiwaameshika mayai yanayozalishwa na mradi wa kuku anaouendesha. |
Mzee Masambu anasema kijana wake alianza na ufugaji wa kuku 100, lakini kwa sasa biashara yake imekuwa kwani anao kuku 200 mchanganyiko, yaani kuku wa mayai na kuku kwa ajili ya nyama. Anasema kwa kilamwezi kijana huyo hutengeneza faida ya takribani shilingi 300,000 kutokana na biashara hiyo, jambo ambalo anaona linamsaidia tofauti na angetelekezwa bila shughuli yoyote kwa kisingizio cha ulemavu wake.
Anaongeza kuwa licha ya ulemavu alionao kijana wake, anakusanya mayai mwenyewe na kuwapa chakula kuku wake, ila wanafamilia humsaidia kufuata chakula cha kuku mjini. Anasema kijana huyo anaweza pia kufanya mauzo ya mradi wake mwenyewe na kupokea fedha halali kwa malipo ambazo anazifahamu hivyo, hilo pia sio tatizo kwake.
Anasema kuwa kwa Baraka anaisaidia kwa kiwango fulani familia yao kutokana na shughuli anazozifanya. "Ni msaada kiasi fulani kwa familia unajua licha ya ulemavu alionao lakini anafanya shughuli na kuingiza kipato, yapo mahitaji ambao akitaka unaweza mnunulia kupitia faida yake kwenye biashara yake tofauti na kwamba angelikuwa akimtegemea mtu kwa kila kitu. Kijana wangu kwa sasa anaweza kuishi na mtu yoyote anayemsaidia kwa baadhi ya mambo hata bila kuwa mzigo, hii ni kutokana na kwamba naye anaweza kufanya baadhi ya shughuli zake na kuingiza kipato kidogo."
Baraka ni mmoja wa vijana wengi wenye ulemavu wa uziwikutoona ambao Shirika la Sense International limeweza kuwasaidia kujitegema kiuchumi na kuwa na mchango katika familia na jamii zinazowazunguka. Uwezo wa kujitegema umewaongezea kujiamini kutokana na thamani yao katika kuongezeka kutokana na mchango wao katika jamii kuongezeka.
Aidha shirika la Sense International linaamini katika uwezo wa watu wenye ulemavu wa uziwikutoona kuwa na mchango katika maeneo ya kazi mathalani katika ajira. Katika kuthibitisha hilo Sense International ikishirikina na serikali ya Tanzania pamoja na Chuo cha Ufundi Stadi cha Yombo linatekeleza mradi wa kuwawezesha vijana wenye ulemavu wa uziwi kutoona na changamoto za mawasiliano kupata elimu ya ufundi stadi na kisha kuwaonganisha na fursa za ajira. Lengo ni kuhakikisha kuwa vijana wenye ulemavu wa uziwikutoona wanashiriki katika soko la ajira. Mradi huu unatekelezwa kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya na mpaka sasa vijana wapatao 17 wamekwisha anza mafunzo katika Chuo Cha Ufundi Stadi cha Yombo.
Kwa mapana zaidi Sense International itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali katika kutoa huduma bora kwa watu wenye ulemavu wa uziwi kutoona. Huduma hizi zinajumuisha utambuzi wa awali wa ulemavu wa uziwikutoona kwa watoto wenye umri wa miaka 0-5 katika vituo mbalimbali vy afya; Utoaji wa mazoezi tiba kwa watoto wanaotambuliwa kuwa na ulemavu wa uziwi kutoona ili kuwawezesha kufikia maendeleo ya ukuaji katika miaka ya awali; Kutoa elimu jumuishi ya ngazi ya msingi kwa watoto wenye ulemavu wa uziwi kutoona na kisha kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi ili kujiongezea kipato na kuwa na mchango katika jamii.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇