LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 18, 2021

TAKUKURU YAAGIZWA KUCHUNGUZA MATAPELI ARDHI KATA PANGANI KIBAHA MJINI


“NAAGIZA TAKUKURU fuatilieni suala la migogoro ya ardhi,” ni kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Kibaha Mjini, ndugu Maulid Bundala alipofanya ziara kutembelea Mtaa wa Vikawe, Kata Pangani kwa lengo la kuzungumza na viongozi na wananchi kuhusu migogoro ya ardhi inayoendelea katika eneo hilo.
Ziara hiyo ambayo ilishirikisha wajumbe wa Kamati ya siasa CCM Wilaya Kibaha Mjini ilifanyika kufuatilia hivi karibuni wananchi kufunga ofisi ya Serikali ya Mtaa huo wa Vikawe Shule kutokana na mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na viongozi wao.

---------- (Pichani ni Mwenyekiti wa CCM Tawi la Vikawe Shule akijieleza mbele ya viongozi wa CCM Wilaya kuhusu mgogoro wa ardhi uliosababisha ofisi ya Serikali ya Mtaa huo kufungwa hivi karibuni kabla ya Mkuu wa Wilaya Kibaha mjini kwenda na kufanikiwa kuifungua).------

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wameshauri vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina wa kuwatambua wanaoendeleza utapeli wa ardhi katika Kata Pangani na kuchukua hatua kwani migogoro inaharibu amani.
“Migogoro ya ardhi ina athari kubwa sana, unakuta mtu anajenga nyumba yake lakini ghafla anaambiwa usiendelee na ujenzi, hiki kiwanja sio chako… mambo kama haya yanawatokea wengi katika Kata hii ya Pangani, wanaofanya utapeli wanafahamika, inadaiwa hawachukuliwi hatua kwa sababu ni mtandao unaonufaisha hadi baadhi ya wakubwa juu, wanatumia rushwa na wengine wanakesha kwa waganga kutafuta dawa za kutapeli watu ardhi,” alisema mkazi mmoja wa Vikawe Shuleni ambaye hakupenda jina lake litajwe.
Kwa upande wake Bi. Zamda Komba, Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM Wilaya Kibaha Mjini alisema Pangani ndio kata inayoongoza kwa migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kibaha Mjini, sifa ambayo sio nzuri, hivyo akashauri jitihada zifanywe kuondokana na sifa hiyo mbaya.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wana hofu kama sifa hii inaweza kuondoka katika Kata Pangani ikiwa baadhi ya viongozi ndio watuhumiwa wa kuendeleza vitendo hivi vya utapeli wa ardhi za wananchi. Aidha yapo madai ya baadhi ya viongozi kuhusika moja kwa moja kuvamia na kuuza ardhi ya Mitamba ambayo ni mali ya Serikali. Mitamba ni enelo lililokuwa limetengwa na Serikali kwa ajili ya kulishia mifugo, kwa sasa halitumiki. Baadhi ya viongozi wanadaiwa kujikatia ardhi watakavyo katika eneo hilo la Serikali wakitumia majina jamaa zao, huku wengine wakisimamia kuliuza kwa watu mbalimbali.
Viongozi ndio walipaswa kuwa kimbilio la wananchi wasitapeliwe lakini hali ni tofauti kwa Kata ya Pangani, kwani baadhi ya viongozi ndio watuhumiwa wakubwa wa uporaji ardhi ya wananchi.
“Kata Pangani ina changamoto nyingi, kwa mfano Shule nyingi zilizoko ikiwamo Shule ya Msingi Kidimu na Sekondari Kidimu, hazina madawati ya kutosha, watoto wanakaa chini, huku matapeli yakivuna mamilioni kwa kuuza ardhi ikiwamo ya Mitamba ambayo ni mali ya Serikali… ni bora wangeelekeza fedha hizo katika maendeleo,” anasema mkazi mwingine wa Vikawe Shule na kushauri mawaziri wa Mifugo na yule wa Ardhi watembelee Kata Pangani ili kuchukua hatua dhidi ya eneo la Mitamba linalouzwa kinyemela na baadhi ya viongozi wasio waaminifu.
Mwenyekiti Bundala alisisitiza TAKUKURU kufanyia kazi jambo hilo ili liweze kuwa na suluhisho la kudumu, huku wananchi wamewashauri TAKUKURU kutomwogopa yeyote hata kama ni kiongozi ili kumaliza migogoro isiyoisha ya ardhi inayoharibu amani katika kata hiyo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages