LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 18, 2021

RAIS SAMIA AFANYA MAZUNGUMZO NA MWENYEKITI WA WILMAR INTERNATIONAL YA SINGAPORE, IKULU, JIJINI DAR ES SALAAM, LEO

Ikulu, Dar es Salaam, leo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Wilmar International ya Singapore Kuok Khoon Hong, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo.


Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, Jaffar Haniu, leo, imesema, Kampuni hiyo yenye Makao Makuu nchini Singapore hufanya shughuli zake katika nchi za Malaysia na Indonesia.


Imesema, katika mazungumzo hayo, Hong ameahidi kuwa kampuni hiyo ipo tayari kupanua uwekezaji wake katika uzalishaji wa mchele na mafuta kwa kuwa mchele wa Tanzania ni bora na wenye soko kubwa duniani na mahitaji ya mafuta ni makubwa ndani ya nchi.


Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Hong amesema Kampuni hiyo imefurahishwa na dhamira ya Rais Samia ya kuwavutia zaidi wawekezaji na kwamba tayari imeshawekeza hapa nchini kiasi cha Dola Milioni 1.5 za Marekani katika Kiwanda cha kusafisha mafuta ya kula, kutengeneza sabuni na tambi ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa takribani Dola Bilioni 1 za Marekani, Barani Afrika.


Kwa sasa kampuni ya Wilmar imekamilisha kujenga kiwanda cha kukoboa mpunga na kufungasha mchele Mkoani Morogoro kitakachokuwa na uwezo wa kukoboa tani 1,000 za mpunga kwa siku na kutoa ajira kwa watu zaidi ya 300.


Akizungumza na mwekezaji huyo Rais Samia amempongeza Hong kwa uwekezaji wake hapa nchini na amemkaribisha kupanua zaidi uwekezaji huo hususan katika uzalishaji na usindikaji wa mafuta ya alizeti, michikichi na kilimo cha umwagiliaji.


Amemueleza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na kampuni hiyo katika uwekezaji huo na ameagiza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango kuandaa andiko la pamoja na kampuni hiyo litakalowezesha ushirikiano huo hususan katika kupata teknolojia, mbegu na mitaji.


"Aidha, Rais Samia ametoa mwito kwa wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini Tanzania hasa katika sekta ya kilimo kwa kuwa Tanzania ina eneo kubwa linalofaa kwa kilimo na ambalo halitumiki ipasavyo", imesema taarifa hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazungumzo yamehudhuriwa na Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda, Balozi wa Tanzania nchini Malaysi Dk. Ramadhan Dau, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Alphayo Kidata.

Picha👇

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Wilmar International ya Singapore Kuok Khoon Hong, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Wilmar International ya Singapore Kuok Khoon Hong, akizungumza yaliyojiri baada ya mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo.(Picha zote na Ikulu)


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages