LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 23, 2021

AFISA MAENDELEO PANGANI ROSE NGALAI AWA KIVUTIO UJENZI KIVUKO CHA MUDA

AFISA Maendeleo Kata ya Pangani, Bi. Rose Ngalai alionekana kuwa ni kivutio kwa wananchi waliofika katika utengenezaji wa kivuko cha muda katika mto mpiji.

Tofauti na wafanyakazi wengi wa Serikali na viongozi ambao huenda katika matukio ya kujitolea bila kufanya kazi au kufanya kazi kidogo na kuacha, Bi. Rose (anayevuta mti, kulia kwake ni Shukrani Mbunda, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi katika Serikali ya Mtaa Mkombozi, Kata Pangani, Halmashauri ya Mji Kibaha, Pwani) alikuja kujitolea akiwa na jembe lake.
“Makubwa haya, huyu mdada ni ofisa wa Serikali halafu amekuja kujitolea na jembe, du” alijisemea kijana mmoja baada ya kumuona Rose akija eneo la kujitolea na jembe lake akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miwale, Allen Lyimo. Bi. Rose mwenyewe alionekana kufurahia kujitolea, huku wengine wakisema ni kawaida kwake kufanya hivyo.
Pichani ni ndugu Merere Mwambene, Mwenyekiti wa CCM Kata Pangani, akiteta jambo na Rose Ngalai.
Wakati watu wanaendelea kumshangaa na jembe lake, Bi. Rose akiwa katika eneo la mto panapotengenezwa ili watu waweze kupita baada ya daraja kufungwa kutokana na kuendelea na ujenzi, alishauri zikatwe nyasi na kufukia eneo mojawapo ili watu waweze kupita.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miwale, Alen Lyimo akisaidiana kubeba matawi ya miti na Rose Ngalai.
“Uko sahihi, alisikika Lyimo akiafikiana na mawazo ya Bi. Rose…” Bi. Rose alichukuana na Shukrani Mbunda, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Serikali ya Mtaa wa Mkombozi kwenda kuanza kukata matawi ya miti kwa ajili ya kuweka katika eneo mojawapo la mto ili kuwezesha wananchi kupita.
Bi. Rose alikuwa ndio mbeba miti na kuileta darajani, huku wananchi wengine wakiungana nae, wengine wakibeba mchanga uliowekwa kwenye mifuko ili kuwezesha wananchi kupita bila kuloa.
Bi. Rose ambaye hivi karibuni aliongezewa cheo kwa kuwa Kaimu Afisa Mtendaji Mtaa wa Miwale, alisababisha baadhi ya wananchi kusema anayo haki ya kupewa madaraka kwa moyo wake aliounyesha kwenye ujenzi wa kivuko hicho cha muda.
Wananchi wengine waliokuwepo katika tukio hilo walifurahishwa na uwepo wa Afisa Maendeleo huyo Kata na kuomba viongozi wengine kuiga mfano wake. Kata ya Pangani kwa sasa haina Afisa Mtendaji baada ya aliyekuwepo kuomba kuhamishwa. Mwisho.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages