Nairobi, Kenya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 04 Mei, 2021 ameanza Ziara Rasmi ya siku 2 nchini Kenya kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta.
Baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi, Mhe. Rais amepokelewa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi ambapo amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake, amepigiwa mizinga 21, amefanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake na kufuatiwa na mazungumzo rasmi.
Baadaye viongozi hao wamezungumza na vyombo vya habari ambapo Mhe. Rais Samia amemshukuru Mhe. Rais Kenyatta kwa mwaliko na mapokezi mazuri yaliyopambwa na wananchi waliojitokeza kwa wingi kumlaki wakati akipita barabarani hali inayothibitisha urafiki, udugu na ujirani mwema wa Tanzania na Kenya.
Mhe. Rais Samia amesema pamoja na kuwepo changamoto mbalimbali katika uchumi, Tanzania imedhamiria kukuza zaidi uchumi wake na hivyo kwa kutambua kuwa Kenya ni nchi inayoshika nafasi ya 5 kwa uwekezaji mkubwa nchini Tanzania na nafasi ya 1 Afrika, anawaalika wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi kutoka Kenya kuwekeza nchini Tanzania kwa manufaa ya pande zote mbili.
Amesema kampuni 513 za Kenya zimewekeza nchini Tanzania mtaji wa Dola za Marekani Bilioni 1.7 (sawa na shilingi za Tanzania Trilioni 3.888) ambazo zimezalisha ajira 51,000 ilihali kampuni 30 za Tanzania zimewekeza nchini Kenya Shilingi za Kenya Bilioni 19.3 (sawa na shilingi za Tanzania Bilioni 410.233), hivyo ameahidi kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi wa Tanzania kuwekeza Kenya.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameongeza kuwa pamoja na kukuza zaidi biashara na uwekezaji, wamekubaliana kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga barabara, kuimarisha usafiri wa majini kupitia Ziwa Victoria, reli na anga pamoja na kushughulikia vikwazo vya biashara ambapo wameagiza Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) ikutane kushughulikia vikwazo hivyo badala ya kuacha mivutano na misuguano ikikwamisha juhudi za kukuza uchumi.
Amebainisha kuwa, wamekubaliana Mawaziri wa Afya wa Tanzania na Kenya kukutana haraka ili kuweka utaratibu wa pamoja wa upimaji wa afya mpakani (ikiwemo upimaji wa virusi vya ugonjwa wa Korona) ili kutowachelewesha wananchi wanaotaka kutoka nchi moja kwenda nyingine wakiwemo wafanyabiashara.
Viongozi hao pia wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Bagamoyo – Tanga – Horohoro – Lungalunga – Mombasa – Malindi (kilometa 454), mradi wa kusafirisha umeme kilovoti 400 kutoka Singida (Tanzania) hadi Isinya (Kenya) na mradi wa bomba la gesi la kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa ambapo wameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano katika mradi huo na utiaji saini wa makubaliano kuhusu utamaduni, sanaa, mwingiliano wa kijamii na urithi wa Kitaifa.
Aidha, Mhe. Rais Samia amekwenda katika viwanja vya Bunge la Kenya ambapo ameweka shada la maua katika kaburi la Muasisi wa Taifa la Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.
Mhe. Rais Samia amemualika Mhe. Rais Kenyatta kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatakayofanyika tarehe 09 Desemba, 2021.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Kenyatta amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kukubali mwaliko wake na amempongeza kwa kupokea kijiti cha kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amemhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania hususani katika uchumi na ameungana nae kuwataka Mawaziri wa Kenya kushirikiana na Mawaziri wenzao wa Tanzania kuondoa vikwazo vyote vya kibiashara ambavyo vinakwamisha kukua kwa uchumi.
Mhe. Rais Kenyatta amesema Tanzania na Kenya ni nchi zenye uhusiano wa kidugu, kirafiki na kihistoria ukiwa umeasisiwa na Muasisi wa Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Muasisi wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta, hivyo amesisitiza kuimarisha ushirikiano na umoja badala ya kila nchi kwenda pekee yake.
Leo jioni Mhe. Rais Samia atahudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇