Na Lydia Lugakila, Bukoba
Watoto wawili na Dreva wa lori aina Scania lenye namba za usajili T351BXG wamenusurika kifo baada ya kufunikwa na shehena ya Saruji iliyokuwa imebebwa na lori, kufuatia lori hilo kupata ajali, leo.
Shehena hiyo ya mifuko ya Saruji iliwafunika baada ya lori hilo mali ya Kampuni ya Magu, lililokuwa limeibeba likitokea Dodoma kuja Bukoba kuacha njia na kuingia kwenye korongo kisha kupinduka baada ya kufeli breki.
Akizungumza kwenye eneo la tukio, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Kagera Thomas Majuto, amesema ajali hiyo imetokea saa 8:50 asubuhi na kumtaja dereva wa lori kuwa ni Rwegasira Devid (41) na watoto kuwa ni Avitus Renald (7 ) na Switbert Nassoro ( 4) wote wakazi wa Bukoba.
Kamanda Majuto amesema, baada ya juhudi za Jeshi la Polisi na Zimamoto kufika eneo la tukio waliwaokoa dereva na watoto hao wakiwa wamejeruhiwa na kuwapeleka katika Hospitali ya Rufani ya mkoa wa Kagera kwa ajili ya matibabu na kwamba hali zao wote zinaendelea vizuri.
Aidha Kamanda huyo amesema eneo ilikotokea ajali ni baya na pamekuwa pakitokea ajali mara kwa mara kutokana na kuwa na mteremko na kwamba Kamati husika ya usalama barabarani itahakikisha inaweka alama zenye kuonyesha alama za mteremko mkali.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo akiwemo Abdalla Muaga na mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Bashir, wameomba serikali kukarabati maeneo mabaya likiwemo eneo la mzunguko 'round about' ambalo limekuwa likisababisha ajali mara kwa mara.
Wananchi wakilitaza lori lililopata ajali na shehena ya saruji iliyokuwa katika lori hilo kumfunika dereva na watoto wawili, leo mjini Bukoba.
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Kagera Thomas Majuto, akiwa kwenye eneo la ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇