Mbinga, Ruvuma
KIJIJI cha Litembo kilichopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kimebarikiwa kuwa na vivutio adimu cha utalii ambavyo huwezi kuviona mahali pengine hapa nchini pengine na duniani kote, anaripoti Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma.
Salvius Nyamajabeni ni Mwenyekiti Baraza la Mila na Utamaduni wa kabila la wamatengo katika kijiji hicho aliyechaguliwa tangu mwaka 1958 anasema, Kijiji hicho kina kivutio ambacho kinawashangaza wengi ambacho anakitaja kuwa ni uwepo wa nyayo ya binadamu wa kale ambayo wananchi wa Litembo wanaamini kuwa ni nyayo ya Yesu.
"Kuna alama ya nyayo ya binadamu yenye vidole ambayo imekanyagwa juu ya jiwe miaka mingi iliyopita, sisi wananchi wa Litembo tunaamini kuwa Yesu amekanyaga kwa sababu haifutiki miaka yote", anasema Nyamajabeni.
Anasema kila mwaka waumini wa Kikristo wanapanda juu kilele cha jiwe la Litembo ambako kuna nyayo hiyo na kwenda kuhiji na kwamba eneo hilo pia limewekwa msalaba.
Mwenyekiti huyo anasema kijiji cha Litembo kina vivutio vingi vya utalii ambavyo havijatangazwa na kufahamika ambapo amelitaja jiwe la Litembo, lina utajiri wa utalii wa kishujaa na kihistoria kutokana na mababu na mabibi takribani 800 waliuwawa na wakoloni wa Kijerumani Machi 4,1902, kutokana na kukataa kutawaliwa.
Amelitaja jiwe ambalo yalifanyika mauaji hayo kuwa linaitwa Litembo, jina ambalo limetokana na kufanana sana na kichwa cha mnyama tembo.
Anasema eneo hilo yalikuwa makazi na maficho ya wazee wakati wa vita dhidi ya Wajerumani ambapo ndani ya jiwe hilo kuna pango refu linalotokea katika Kijiji cha Maguu wilayani Mbinga.
Inaelezwa ndani ya pango hilo kuna Wanyama wakali, nyoka, maji mengi, pia inadaiwa kuna madini ya zebaki na samani za chuma.
Katibu wa Baraza la Mila na Utamaduni Kata ya Litembo, Bruno Tembo anasema mashujaa hao 800 baada ya kuuawa walizikwa katika makaburi ya Pamoja ya watu 25 katika Kijiji cha Litembo na kwamba ili kuwakumbuka mashujaa hao mnara wa makumbusho umejengwa kwenye maeneo ya jiwe la Litembo na kwamba kila mwaka Novemba 28 yanafanyika maadhimisho ya kuwakumbuka wazee 800 waliopambana na wajerumani.
Mwenyekiti Mstaafu wa kijiji cha Litembo Paulo Mwingira anasema serikali ya kijiji hicho kwa kushirikiana na wazee wa mila wa kabila la wamatengo wamejipanga kuhakikisha kuwa vivutio vyote vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo katika eneo hilo vinalindwa na kuendelezwa kwa ajili ya urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Afisa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema, wamedhamiria kuvitangaza vivutio vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo eneo la Litembo ili watalii wengi waweze kufika na kuona namna mababu zetu walivyoshiriki katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni wa kijerumani.
Alama ya unyayo wa binadamu aliyekanyaga kwenye mwamba wa jiwe Litembo lililopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ambalo inasadikiwa na wenyeji wa eneo hilo kuwa ni unyayo wa Yesu.Mwamba wa jiwe Limbo, ambao unyayo huo upo juu yake
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇