Arnatouglou, Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla ameanza rasrmi majukumu yake kwa kukutana na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es salaam.
RC Makalla amekutana na Wazee hao, leo katika ukumbi wa Arnatouglou, na kueleza kwamba ameweka utaratibu wa kufanya kikao na wazee hao kila baada ya miezi mitatu.
Amesema anatambua thamani na mchango wa Wazee Katika jamii, hivyo ameona ni vyema kuanza majukumu yake kwa kukutana nao ili kuchota busara na baraka zao kwani anatambua Wazee ni hazina muhimu.
RC Makalla, amesema Katika kutatua kero na changamoto za Wananchi amepanga kuanza ziara ya Kata kwa Kata, hivyo amewahakikishia wananchi kuwa anayo dhamira ya dhati kuzipatia majibu kero walizonazo.
Amesema, kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni mkoa mkubwa na wenye kutoa taswira ya nchi nzima kwenye kila nyanja, amejipanga kuhakikisha Jiji linakuwa shwari na watu wanafanya shughuli zao pasipo usumbufu wowote kulingana na maono na matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wao Wazee walioshiriki kikao hicho wamemshukuru na kumpongeza RC Makalla kwa namna anavyoheshimu Wazee na wamemuahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha katika majukumu yake.
Wazee hao wamesema wana imani kubwa na Mkuu huyo wa mkoa, kwakuwa wasifu wake wa uongozi unaonyesha kila alipopita amekuwa akiacha alama hivyo wanaamini atafanya mambo makubwa na mazuri katika mkoa wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇